Majlisi ya maombolezo ya Tasu'a ya Imam Hussein (a.s) imefanyika katika Msikiti wa Hawzah ya Al-Hadi(as), ambapo wanafunzi, walimu na baadhi ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s) walikusanyika kuhuisha kumbukumbu za Karbala na kujifunza kuhusu nafasi ya Imam Hussein (a.s) na Abul-Fadhli al-Abbas (a.s) katika historia ya Uislamu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) –ABNA–, Majlisi ya maombolezo ya Tasu'a ya Imam Hussein (a.s) imefanyika asubuhi ya Alhamisi, tarehe 25 Juni 2026, katika ukumbi wa sala wa Shule ya Al-Hadi, ikiwakutanisha wanafunzi, walimu pamoja na baadhi ya waumini wa Kishia.
Katika hotuba yake, Sheikh Abdulrashid Shu'aib alizungumzia utabiri wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuhusu kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (a.s), akieleza hadithi maarufu ya Mtume isemayo: "Hussein ni sehemu yangu na mimi ni sehemu ya Hussein."
Aidha, alisisitiza kwamba kumpenda na kumheshimu Imam Hussein (a.s.) ni sehemu ya kumpenda na kumheshimu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), na kwamba uadui dhidi ya Imam Hussein (a.s.) ni uadui dhidi ya Mtume (s.a.w.w.).
Mhadhiri huyo pia alieleza maisha na sifa za Abul-Fadhli al-Abbas (a.s.), akizungumzia nafasi yake katika Karbala, hususan juhudi zake za kutafuta maji kwa ajili ya watoto na watu wa nyumba ya Imam Hussein (a.s.), pamoja na baadhi ya lakabu zake mashuhuri kama Qamar Bani Hashim na Mbeba Bendera wa Karbala.
Kwa upande wake, Sheikh Abdulrashid Yusuf alizungumzia nafasi ya siku ya Tasu'a katika historia ya Karbala, akieleza hekima na manufaa ya kiroho yanayopatikana kupitia maombolezo ya Imam Hussein (a.s). Pia alisisitiza kuwa msiba wa Imam Hussein (a.s.) ni miongoni mwa misiba mikubwa zaidi katika historia ya mwanadamu na kwamba kumbukumbu zake zinaendelea kuhuisha dhamiri za waumini na kuwafundisha kusimama dhidi ya dhulma.
Aidha, alizungumzia fadhila za Imam Hussein (a.s.) zilizotajwa katika Qur'ani Tukufu, hususan katika Surah Al-Fajr, pamoja na kujibu baadhi ya hoja za wanaopinga maombolezo ya Imam Hussein (a.s.).
Majlisi hiyo pia ilipambwa na usomaji wa mashairi ya maombolezo yaliyowasilishwa na wanafunzi Amin Wilson na Mahd Abdulrahman, yaliyoibua hisia za huzuni na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s).
Washiriki wa hafla hiyo walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ujumbe wa Karbala, kuimarisha mapenzi kwa Imam Hussein (a.s) na kujifunza kutoka kwa ujasiri, uaminifu na kujitolea kwa Abul-Fadhli al-Abbas (a.s.) katika kutetea haki na dini ya Mwenyezi Mungu.
Your Comment