Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala, ameungana na waumini katika zoezi la usafi lililofanyika Kigogo, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (a.s) na kueneza ujumbe wa huduma kwa jamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (AS) –ABNA–, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala, leo ameshiriki katika zoezi la usafi lililofanyika katika maeneo ya Kigogo Post, kuanzia Njia Panda hadi Kigogo Mwisho, jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo limefanyika katika kuadhimisha kumbukumbu ya kumuomboleza na kumuenzi mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Hussein (a.s), aliyeuawa shahidi katika ardhi ya Karbala.
Washiriki wa shughuli hiyo walisisitiza kuwa maadhimisho ya Ashura hayajikiti tu katika ibada na maombolezo, bali pia yanajumuisha huduma kwa jamii na kuhamasisha maadili ya usafi, mshikamano na kujitolea kwa manufaa ya watu wote.
Maulana Sheikh Hemed Jalala alieleza kuwa ujumbe wa Imam Hussein (a.s) unawataka Waislamu na wanadamu wote kusimamia haki, kuendeleza umoja na kushiriki katika shughuli za kijamii zinazochangia ustawi wa jamii.
Zoezi hilo lilihudhuriwa na viongozi wa dini, waumini na wananchi wa eneo hilo, ambao walionesha mshikamano wao katika kuenzi misingi ya Karbala kupitia matendo ya huduma kwa jamii.
Your Comment