Wanafunzi wa Hawzah ya Mabanati ya Hazrat Zainab (sa) iliyopo Kigamboni Jijini Dar-es-salaam - Tanzania, pamoja wasimamizi wao, walishiriki katika kuhuisha kisomo cha Dua ya Tawasuli kilichoandaliwa na Hawzah hiyo, ambapo walikumbushwa nafasi ya dua hiyo katika kuimarisha imani, kuongeza matumaini na kuimarisha uhusiano wa Waumini na Mwenyezi Mungu kupitia Ahlul-Bayt (as).
Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Hawzah ya Wasichana imeendesha kwa mafanikio hafla ya Kiroho ya kuhuisha kisomo cha Dua ya Tawasuli, sambamba na mawaidha yaliyoeleza umuhimu wa dua hiyo katika maisha ya kiroho ya Muislamu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Wanafunzi 144 pamoja na wasimamizi wao, ambapo washiriki walisoma Dua ya Tawasuli kwa unyenyekevu na kuelekezwa kuhusu nafasi ya Dua ya Tawassuli kwa Ahlul-Bayt (as) kama njia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kuimarisha imani, kustahimili mitihani ya maisha na kuomba msaada Wake katika mambo mbalimbali.
Mmoja wa Mabanati alitoa mawaidha mafupi akisisitiza kuwa Dua ya Tawasuli ni miongoni mwa dua zinazowajenga Waumini Kiroho, huku ikiimarisha mapenzi na kushikamana na Ahlul-Bayt (as), ambao Mwenyezi Mungu Amewateua kuwa viongozi wa uongofu kwa Umma wa Kiislamu.
Washiriki pia walimwomba Mwenyezi Mungu Awalinde Waislamu duniani kote, Awajaalie wanafunzi mafanikio katika safari yao ya elimu, Awaondolee waumini matatizo mbalimbali na Aharakishe kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.t.f.s).
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa dua na maombi mbalimbali, huku ikiacha athari chanya za kiroho na kuhimiza kuendelezwa kwa programu za ibada na malezi ya Kiislamu katika taasisi za elimu.
Maoni yako