Maelfu ya Waislamu na wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) wameendelea kushiriki matembezi ya Arubaini katika Jimbo la Kano nchini Nigeria, wakihuisha ujumbe wa A'shura na kuwakumbuka Mashahidi wa Karbala pamoja na waathiriwa wa shambulio la mwaka 2014.

4 Agosti 2026 - 14:57

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Maelfu ya Waislamu na wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) wameendelea kushiriki matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) katika Jimbo la Kano, Nigeria, chini ya uratibu wa wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky. Matembezi hayo yanafanyika kwa utulivu na mpangilio mzuri huku washiriki wakionesha mapenzi yao kwa Ahlul-Bayt (as) na kuhuisha ujumbe wa Ashura.
 
Katika siku ya pili na ya tatu ya matembezi hayo, yaliyofanyika Ijumaa na Jumamosi, washiriki walianza safari yao baada ya kuswali Swala ya Alfajiri na kupata kifungua kinywa katika maeneo yao ya mapumziko.
 
Siku ya pili ya matembezi ilianza kutoka mji wa Qarfi, ambapo baada ya kutembea kwa umbali uliopangwa, washiriki walifika karibu na mji wa Dakasoye na kushiriki hafla ya kuwaenzi mashahidi wa shambulio la mlipuko wa mwaka 2014, lililowalenga washiriki wa matembezi ya Arubaini katika eneo la Kano.
 
Katika hafla hiyo, Sheikh Sanusi Abdulkadir alitoa nasaha akieleza mafunzo yanayotokana na tukio hilo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwakumbuka mashahidi na kuwaombea waliofariki katika shambulio hilo.
 
Katika safari yote, waombolezaji walisoma tenzi na marsiya za kuomboleza shahada ya Imam Hussein (as) na mashahidi wa Karbala, huku wakisisitiza mshikamano wao na mafunzo ya Ashura ya kujitolea, subira, uaminifu na kusimama imara katika kutetea haki.
 
Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, matembezi hayo yamewakutanisha maelfu ya washiriki kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Kano, Maiduguri, Azare, Nguru, Jigawa na maeneo mengine ya Nigeria.
 
Matembezi ya Arubaini katika Jimbo la Kano yameendelea kuwa ishara ya upendo na utii wa Waislamu kwa Ahlul-Bayt (as), pamoja na fursa ya kuhuisha ahadi ya kufuata misingi ya Imam Hussein (as) ya kusimamia haki, kupinga dhuluma na kuendeleza maadili ya Kiislamu.

Maoni yako

You are replying to: .
captcha