Polisi ya Pakistani imesema leo Ijumaa kuwa "mlipuko huo ulitokea katika msikiti wa shule ya kidini inayojulikana kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa Taliban wa Afghanistan katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, kaskazini magharibi mwa Pakistani, na kuua watu watano na kujeruhi wengine kadhaa."
Ripoti zinasema, Maulana Hamidul Haq, mkuu wa chama cha kisiasa cha Haqqaniyya na kituo cha kidini cha kundi hilo pia ameuawa katika shambulio la kujilipua kwa bomu adhuhuri ya Ijumaa ya leo.
Maulana Hamidul Haq alichukua uongozi wa chama cha siasa cha Haqqani baada ya kuuawa baba yake, Maulana Samiul Haq. Jumuiya ya Haqqani ni moja ya vituo maarufu vya kidini vya kundi la Deobandi, na viongozi wengi wa Taliban wa Afghanistan na Taliban Pakistani, wakiwemo viongozi wa mtandao wa Haqqani, wamepata elimu katika shule za jumuiya hiyo.
Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya serikali ya Pakistan na makundi ya kigaidi, mashambulizi ya makundi hayo yameongezeka katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa na maeneo ya mpakani kati ya Pakistan na Afghanistan.
Taasisi ya Pakistani ya Utafiti wa Amani (PIPS) yenye makao yake makuu mjini Islamabad imesema katika ripoti yake kwamba watu wasiopungua 100 waliuawa katika mashambulizi ya kigaidi mwezi Oktoba pekee, ikiwa ni ongezeko la asilimia 100 kutoka vifo 50 mwezi Septemba mwaka jana.
342/
