Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametuma ujumbe wake wa salamu za Ramadhani na kutaka kipindi hicho cha takribani siku 30 kitumike kuleta amani na kuongoza kuelekea dunia yenye haki na huruma zaidi.
Sehemu moja ya ujumbe huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inasema: Natuma salamu zangu za dhati wakati huu mamilioni ya Waislamu duniani kote wakielekea kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Guterres amesema: "Ramadhani inabeba maadili ya amani, upendo, huruma na ukarimu. Ni kipindi cha kutafakari na kusali, ni fursa ya kuwa pamoja na kuinuana."
Hata Hata hivyo amesema: “Cha kusikitisha, wengi watafunga mwezi huu huku wakikabiliwa na mizozo, ukimbizi na hofu. Fikra zangu na moyo wangu viko nao – kuanzia wananchi wa Afghanistan hadi Sahel, kuanzia Pembe ya Afrika hadi Syria na kwingineko. Na ningependa kutoa ujumbe maalumu wa mshikamano na usaidizi kwa wale wanaokumbwa na machungu na zahma huko Gaza.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha anasema kwamba, katika zama hizi za majaribu, mfungo wa Ramadhani unakuwa nguzo ya matumaini na kumbusho la utu wa pamoja wa binadamu.
Aidha amesema: “Hebu na tuhamasike kwa ajili ya kuponya migawanyiko, kusaidia wenye uhitaji, na tufanye kazi kwa pamoja kwa usalama na utu wa kila mwanachama wa familia hii ya binadamu na mwezi huu mtukufu ulete amani na utuongoze kuelekea dunia yenye haki na huruma zaidi. Ramadhani njema.”
342/
