4 Machi 2025 - 23:26
Source: Parstoday
Hamas: Hatua ya Pili ya Usitishaji Mapigano Gaza ni njia pekee ya kuachiliwa mateka wa Israel

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ameulaumu utawala haramu wa Israel kwa kutaka kurejesha uvamizi wake dhidi ya Gaza na kukwepa makubaliano ya usitishaji mapigano, akisisitiza kuwa njia pekee ya kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka wa Israel ni kuanza hatua ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Osama Hamdan alisema Jumatatu kwamba:"Tunasisitiza kuwa njia pekee ya kuwaachilia wafungwa wa utawala vamizi ni kushikamana na makubaliano na kuanza mara moja mazungumzo ya kuingia katika hatua ya pili, na utawala uvamizi lazima uahidi kutimiza wajibu wake."

Hamdan amesema kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na serikali yake wanabeba dhamana kamili kwa kuzorotesha makubaliano hayo.

Amekemea hatua ya Israel kukiuka awamu ya kwanza ya mapatano ya usitishaji vita. Ametaja baadhi ya vitendo vya ukiukaji mapatano vilivyotekelezwa na Israel kuwa ni pamoja na  hujuma za anga  mara 210, kuwazuia wakimbizi wa ndani kurejea makwao, kua Wapalestina 116, kucheleweshwa zoezi la kuachiliwa wafungwa, na kuzuia biashara na misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.

Israel pia imezuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza baada ya kumalizika kwa hatua ya kwanza ya usitishaji mapigano bila makubaliano juu ya hatua ya pili.

Hamdan amesisitiza kuwa Hamas imejitolea kutekeleza hatua ya pili ya makubaliano ya usitishaji mapigano.

Aidha, alikosoa msaada usio na masharti wa Marekani kwa Israel, akisema kuwa unatishia amani ya kikanda na usalama wa dunia nzima.

Katika maelezo mengine, Hamdan ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuihimiza Israel kuruhusu misaada muhimu kuingia Gaza.

Hatua ya kwanza ya usitishaji mapigano Gaza ilimalizika bila mafanikio makubwa, licha ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Cairo.

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanajumuisha hatua tatu za wiki sita kila moja, zinazolenga kusaidia juhudi za kibinadamu, kuachiliwa mateka na kuondolewa kwa wanajeshi vamizi wa Israel walioko Gaza.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha