Taarifa zinaeleza kuwa Membe alipata changamoto ya kifua na kupelekwa alfajiri ya leo hospitalini hapo na baadaye kufariki dunia.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha hospitali ya Kairuki, Arafa Juba amesema: "Membe aliletwa hospitalini leo asubuhi na akapatiwa matibabu na wataalamu kama ilivyo kawaida mgonjwa anapokuja hospitali, lakini Mungu alimpenda zaidi akafariki saa mbili asubuhi.”
Ripoti kutoka kwa aliyekuwa Msaidizi wake, Allan Kiluvya zimesema, Membe aliugua kwa muda mfupi na kukimbizwa hospitalini, Ijumaa Alfajiri na baadaye akafariki dunia.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ametoa salamu za rambirambi kwa familia kutokana na msiba huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi. Pole kwa familia, ndugu, jamaa & marafiki. Mungu amweke mahali pema", umesema ujumbe wa Rais Samia.
Bernard Kamilius Membe alihudumu katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kati ya mwaka 2007 hadi 2015, wakati wa uongozi wa rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Membe aligombea urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo alichojiunga nacho Julai 15, 2020 miezi kadhaa baada ya kufukuzwa kwenye chama tawala cha CCM.
Mei 29 mwaka jana waziri huyo wa zamani wa mambo ya nchi nje wa Tanzania alikaribishwa tena ndani ya CCM baada ya miaka miwili aliyoishi nje ya chama hicho.
342/