Misingi hii imeelezwa kwa uwazi ndani ya Qur'an Tukufu, Hadithi za Maasumina (amani iwe juu yao) na maisha ya kivitendo (sirah) ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao).
Katika makala hii, kwa kutumia vyanzo hivi, tutajadili kanuni za lishe bora katika mtazamo wa kidini.
1. Epuka kula kupita kiasi (katika lishe).
Moja ya kanuni muhimu za lishe katika Uislamu ni kula kwa wastani. Quran Tukufu inataja kwa uwazi suala hili katika Aya hii Tukufu:
«وَکُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا یُحِبُّ الْمُسْرِفِینَ»
“Kuleni na kunyweni, wala msifanye israfu / ubadhirifu, kwani Mwenyezi Mungu hapendi wafanyao israfu / ubadhirifu”.
(Surah al-A’raf, Aya ya 31).
Aya hii inaonyesha msisitizo wa Uislamu katika kujiepusha na ulaji na unywaji wa kupindukia.
Imam Ali (Amani iwe juu yake) pia alisema katika suala hili:
«المعدة بیت کل داء والحمية رأس کل دواء»
Tafsiri:
"Tumbo ni nyumba ya magonjwa yote; na kujizuia ni matibabu bora zaidi."
(Nahj al-Balagha, Hikmat 11).
2. Kuchagua kula chakula cha halali na safi:
Kanuni nyingine ya msingi katika lishe bora ya Kiislamu ni kusisitiza matumizi ya chakula halali na safi. Imeelezwa kwa uwazi kabisa ndani ya Qur'an Tukufu:
«یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا کُلُوا مِنْ طَیِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاکُمْ وَاشْکُرُوا للهِ»
"Enyi mlioamini! Kuleni katika vile vizuri tulivyo kuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu." (Surat al-Baqarah, Aya ya 172).
Chakula cha halali na safi sio tu kina athari nzuri juu ya afya ya mwili, lakini pia kina athari kubwa juu ya nafsi na tabia ya Binadamu.
Imetajwa katika hadithi za Maasumina kwamba chakula cha halali ni miongoni mwa mambo ya kukubaliwa kwa sala na ibada.
Imamu Sadiq (amani iwe juu yake) anasema:
«طلب الحلال فریضة على کل مسلم»
"Ni wajibu kwa kila Muislamu kutafuta riziki ya halali."
(Wasail - al-Shia, Juzuu ya 17, Ukurasa wa 59).
-
Kauli hii inaonyesha kwamba kuzingatia ubora wa chakula halali kunachukuliwa kuwa ni miongoni mwa faradhi za kidini na kuna athari kubwa katika elimu ya maadili na kiroho ya Waislamu.
3. Kuzingatia wakati na njia / namna ya kula.
Kuzingatia adabu za ulaji pia ni moja ya vipengele muhimu vya lishe bora katika Uislamu.
Maasumina (amani iwe juu yao), wamesisitiza sana juu ya wakati wa kula na namna ya ulaji bora wa chakula.
Moja ya mapendekezo hayo ni kuanza kula chakula kwa Jina la Mwenyezi Mungu na katika hali ya utulivu.
Imamu Sadiq (Amani iwe juu yake) anasema:
《اذكر الله على الطعام ولا تأكل بشراهة》
Tafsiri:
"Kumbuka kulitaja Jina la Mwenyezi Mungu juu ya chakula / wakati wa kutaka kula; na wala usile kwa pupa."
(Al-Kafi, Juzuu ya 6, Ukurasa wa 269).
-
Miongoni mwa mapendekezo mengine yanayohusiana na njia bora ya kula, ni kula kwa kutumia mkono wa kulia na kutokula ukiwa umesimama, jambo hilo limetajwa katika Hadithi.
Mtume wetu Mtukufu (s.a.w.w) amesema:
«اذا أکل أحدکم فلیأکل بیده الیمنى و لیشرَب بها»
"Wakati wowote mtu yeyote miongoni mwenu akila, basi na ale kwa mkono wake wa kulia na kunywa vile vile kwa mkono wake wa kulia".
(Wasail al-Shia, Juzuu ya 16, Ukurasa wa 475).
-
Maagizo haya yanayoonekana kuwa rahisi husaidia kudumisha adabu na utulivu katika kula na kusaidia afya ya mwili na akili ya mtu.
4. Mkazo juu ya baadhi ya vyakula muhimu.
Katika vyanzo vya kidini, vyakula vingine vinapendekezwa hasa kwa kuzingatia kuwa matumizi yake ni ya faida kwa afya ya kimwili na kiroho.
Tende, maziwa, asali na zeituni, vinaweza kutajwa kati ya vyakula hivyo bora zaidi vinavyopendekezwa kuliwa mara kwa mara.
Quran Tukufu inasema kuhusu mzeituni:
«یُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَارَکَةٍ زَیْتُونَةٍ لَّا شَرْقِیَّةٍ وَلَا غَرْبِیَّةٍ»
"Imeangaziwa kutoka kwa mzeituni uliobarikiwa, ambao hauko mashariki wala magharibi."
(Surah al-Noor, Aya ya 35).
-
Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) pia alisema kuhusu Tende:
«البیت الذي فیه تمر لا یجوع أهله»
"Nyumba ambayo kuna tende ndani yake, watu wake hawapatwi njaa."
(Bihar al-An'war, Juzuu ya 66, Ukurasa wa 157).
-
Mapendekezo haya yanaonyesha jukumu la vyakula maalum katika kutoa nishati na virutubisho muhimu kwa mwili wa Mwanadamu.
5. Saumu na faida zake
Saumu ni moja ya ibada muhimu sana na wakati huo huo inakuwa moja ya njia muhimu za kudumisha na kuimarisha afya ya mwili na akili katika Uislamu.
Qur'an Tukufu inasema kuhusu kufunga:
«یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا کُتِبَ عَلَیْکُمُ الصِّیَامُ کَمَا کُتِبَ عَلَى الَّذِینَ مِن قَبْلِکُمْ لَعَلَّکُمْ تَتَّقُونَ»
Tafsiri:
"Enyi mlioamini, imekuwa ni wajibu kwenu kufunga kama ilivyokuwa wajibu kwa waliokuwa kabla yenu, ili mpate kuwa wacha Mungu."
(Surat Al-Baqarah: Aya ya 183).
-
Ikiwa kama njia ya kuimarisha Ucha Mungu na kujidhibiti, funga huwasaidia watu wote (Waislamu wanaofunga) kudhibiti matamanio yao, na pia ina faida nyingi za kimwili.
Kufunga kunaupa mwili nafasi ya kupumzika na kuimarisha mfumo wa usagaji chakula na kuusafisha mwili.
Kanuni za lishe sahihi katika vyanzo vya dini ya Kiislamu, kwa kutoa msisitizo juu ya kiasi cha kula, na kutumia (kula) chakula cha halali na safi, na kuzingatia tabia bora na nzuri za kunywa na kula vyakula muhimu, zinahakikisha (kanuni hizo) upatikanaji wa afya ya mwili na roho ya Mwanadamu.
Kanuni hizo sio tu kwamba zinasaidia kuboresha hali ya kimwili, lakini pia husababisha kumkuza na kumuimarisha mwanadamu kiroho na kiucha Mungu kwa kuunda usawa katika maisha yake na kudhibiti tamaa zake za kimwili.
Kufuata mapendekezo haya katika maisha ya kila siku, kama Muislamu, kunaweza kumhakikishia Mwanadamu afya ya mwili na roho na ukaribu wake kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t).
------------
Vyanzo:
1. Qur'an Tukufu, Surah al-A'raf, Aya ya 31.
2. Qur'an Tukufu, Surah al-Baqarah, Aya ya 172.
3. Nahjul al-Balagha, Hikmat 11.
4. Bihar al-An'war, Allameh Majlisi, Juzuu ya 66.
5. Wasail al-Shia, Juzuu ya 17.