Wasiwasi huu umeibuka baada ya kukamatwa Mahmoud Khalil, ambaye ni miongoni mwa watu mashuhuri katika maandamano ya wanafunzi wanaotetea Palestina katika Chuo Kikuu cha Columbia katika Jimbo la New York, Marekani. Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani imemkamata Khalil na kufuta kadi yake ya ukaazi halali inayojulikana kwa jina la Green Card kwa madai kuwa anaiunga mkono Hamas, kundi ambalo Marekani imelitataja kuwa la kigaidi. Hatua hii imezidisha hatari ya kufukuzwa mwanafunzi huyu wa Palestina kutoka Chuo Kikuu cha Columbia.
Mahmoud Khalil alikuwa na nafasi muhimu wakati wa maandamano makubwa ya watetezi wa Palestina katika baadhi ya vyuo vikuu vya Marekani, kikiwemo Chuo Kikuu cha Columbia, na alijulikana kama mpatanishi kati ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana na utawala wa chuo hicho. Mwaka jana, yeye na kundi kubwa la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia walifanya maandamano na mgomo mkubwa kwenye chuo hicho kupinga vita na mauaji ya jeshi la Israel dhidi ya watu wa Gaza huko Wapalestina. Wanafunzi waliokuwa wakiandamana waliwataka maafisa wa chuo hicho kukata ushirikiano wa kifedha na kiutafiti na serikali ya Israel na taasisi za elimu za utawala huo katili ili kupinga mauaji ya Gaza. Wito huo ulikataliwa na maafisa na usimamizi wa Chuo Kikuu cha Columbia, na badala yake waandamanaji hao walipachikwa tuhuma kuwa wanachuki dhidi ya Wayahudi yaani anti-Semitism. Hii ni licha ya kwamba, miongoni mwa wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina, walikuwepo pia wanafunzi wa Kiyahudi walioitambua serikali ya Israel kuwa inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.
Sasa, miezi kadhaa baada ya maandamano hayo yaliyopanuka na kusababisha ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya dola dhidi ya wanafunzi vyuo vikuu, utawala mpya wa Marekani unajaribu kuwatisha na kuwakandamiza wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina kwa kisingizio cha kukabiliana na wafuasi wa Hamas. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, juhudi kama hizi zilifanywa pia katika utawala uliopita wa Marekani kwa kuwapiga kalamu nyekundu marais wa vyuo vikuu vya Columbia na Pennsylvania, lakini katika utawala wa sasa, Rais wa Marekani Donald Trump amezidisha hatua hizi za ukandamizaji wa wapinzani wa mauaji yanayofanywa na Israel. Hivi majuzi alitangaza uamuzi wake wa kuwafukuza Marekani wanafunzi wa kigeni wanaoitetea Palestina na hata kufikia hatua ya kutishia kwamba, wanafunzi wa Marekani wanaoiunga mkono Palestina wanapaswa pia kufukuzwa katika vyuo vikuu na kufungwa jela. Vitisho hivyo havikuishia hapo, bali katika hatua iliyozusha mjadala mkubwa, serikali ya Marekani ilifuta kandarasi za serikali zenye thamani ya dola milioni 400 na Chuo Kikuu cha Columbia, kwa kisingizio kwamba maafisa wa chuo hicho hawatilii maanani kile kilichoidaiwa ni chuki dhidi ya Wayahudi. Maafisa wa serikali ya Marekani wanatarajia kwamba, watafanikiwa kuzuia maandamano yoyote ya wanafunzi nchini humo dhidi ya mauaji ya Israel kwa kuzidisha mashinikizo ya kifedha kwa vyuo vikuu.
Maafisa usalama wa Marekani wakikandamiza harakati ya wanafunzi wanaopinga mauaji ya Israel huko Palestina.
Vitendo hivi vimekabiliwa na malalamiko ndani ya chuo hicho na vilevile katika duru za kisiasa za Marekani. Baadhi wanaamini kwamba, Mahmoud Khalil aliwaunga mkono Wapalestina na hakutoa maoni yoyote ya umma kuhusiana na harakati ya Hamas. Wakosoaji wengine wanaona kwamba, kukamatwa na kuandamwa mwanaharakati huyu na wanafunzi wengine ni jaribio la kuwatisha watetezi wa Palestina nchini Marekani, ambao watakabiliwa na shutuma na hatua kali za kiusalama ikiwa watang'ang'ania misimamo yao.
Kundi jingine la wachambuzi wa mambo linasema, ukandamizaji huo ni njia ya kutishia vuguvugu la wanafunzi nchini Marekani ili lisiandamane na kupinga baadhi ya sera za serikali ya sasa katika siku zijazo. Vilevile wanazitaja hatua za kiusalama zilizochukuliwa dhidi ya Mahmoud Khalil kuwa ni ukiukaji wa Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, ambayo yanadhamini uhuru wa kujieleza.
342/
Your Comment