Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA- Leo hii, Siku ya Jumamosi, Tarehe: 14 Tir 1404 Shamsia, Sawa na Tarehe : 5 Julai, 2025, na Tarehe: 9 Muharram, 1447Hijria, Majlisi ya Maombolezi ya Aba Abdillah Al-Hussein (as) na Mashahidi wa Karbala, sambamba na kuhuisha mnasaba wa Tasu'a, imefanyika katika Madrasa ya Wasicha wa Kiislamu ya Hazart Zainab (sa), Kigamboni - Dar-es-Salaam - Tanzania. Khatiba wa Majlisi hii Tukufu: Ustadhat Maimuna, ambaye alizungumzia mada muhimu kuhusiana na sifa njema za Masahaba wa Imam Hussein (as). Mada hiyo ilibeba anuani hii maridhawa: "Nafasi ya Imam Hussein (a.s) kwa Masahaba wake".
Katika Khutba hii adhimu, mzungumzaji alieleza kwa undani kwamba Imam Hussein (a.s) alikuwa na nafasi ya kipekee mbele ya Mwenyezi Mungu na Mjumbe wake Muhammad (s.a.w.w), na vivyo hivyo, alikuwa anathaminiwa sana Masahaba wake. Masahaba wa Imam Hussein (a.s) walikuwa watu wa imani ya kweli na waliokuwa na utulivu wa moyo kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Walikuwa waaminifu mno na walionesha mwenendo mzuri sana wakati wote wa uhai wao mpaka mwisho wa uhai wao.
Imam Hussein (a.s) aliishi na Masahaba wake kwa maelewano na mapenzi makubwa. Mara kwa mara, alikuwa akiwaambia kuhusu mustakabali wao mzuri mbele ya Allah (s.w.t). Kwa mfano, katika siku ya Tisa ya Muharram (Tasu'a), Imam aliwaambia Masahaba wake kwamba malipo yao mbele ya Mwenyezi Mungu ni makubwa mno. Kisha akawaambia kuwa kila mmoja ana uhuru wa kubaki au kuondoka.
Licha ya hayo, wote walimjibu kwa uaminifu na ujasiri wakisema: "Tutaendelea kuwa pamoja na wewe hadi mwisho, hadi mwisho wa maisha yetu, hadi tufikie (daraja ya) Shahada. Kamwe hatutakuacha peke yako."
Tanbihi:
Kama tuloivyodokeza hapo juu, Majlisi hii imefanyika kwa kuandaliwa na kuratibiwa na Wanafuzi wa Madrasa ya Wasichana wa Kiislamu, Madrasat Hazarat Zainab (sa), Mwenyezi Mungu awahifadhi na aendelee kuwadumisha katika kuwapenda na kuwafuata: Imam Hussein (as) na Ahlu Bayt Rasulillah (amani iwe juu yao).
Your Comment