1 Januari 2026 - 23:12
Lengo kuu la utawala wa Amirul-Mu’minin (a.s) ni kuwaongoza wanadamu / mpaka kati ya uhuru wa kujieleza na vitendo dhidi ya usalama wa umma

Mheshimiwa Sayyid Mujtaba Nourmofidi, Rais wa Taasisi ya Utafiti wa Fiqhi ya Kisasa, alipohudhuria Shirika la Habari la ABNA, alichambua mada ya: “Fiqhi ya kisiasa katika kuweka mipaka kati ya uhuru wa kujieleza na ukosoaji halali, dhidi ya uasi na vitendo vinavyohatarisha usalama wa umma katika utawala wa Imam Ali (a.s)”.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Sayyid Mujtaba Nourmofidi alieleza kuwa suala la uhusiano kati ya uhuru wa kujieleza na mipaka ya ukosoaji halali dhidi ya vitendo vinavyohatarisha usalama wa umma ni miongoni mwa maswali ya msingi kabisa katika fiqhi ya kisiasa, ambalo limekuwepo tangu zamani na hadi leo linahesabiwa kuwa kipimo cha uhalali wa tawala, hasa katika zama za kisasa.


Asili ya swali na umuhimu wake katika fiqhi ya kisiasa
Nourmofidi alisema: Mtawala na mfumo wa utawala daima hukutana na wapinzani. Swali kuu ni: je, mtawala anapaswa kushughulikaje na wapinzani wake? Katika madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s), ambayo utawala wake umejengwa juu ya mafundisho yao, swali hili lina nafasi ya kipekee. Ili kupata jibu sahihi, ni lazima kurejea vyanzo vya msingi, hasa sira (mwenendo wa vitendo) wa Amirul-Mu’minin Ali (a.s). Sira hii si simulizi la kihistoria tu, bali ni nadharia ya kisiasa yenye mwelekeo na mwongozo, hata kwa mifumo ya kisasa inayojitambulisha kama demokrasia za kiliberali.


Aliongeza kuwa Imam Ali (a.s) katika kipindi cha utawala wake alikabiliana na makundi tofauti ya wapinzani, na aina ya msimamo wake kwa kila kundi ilikuwa tofauti; kuanzia uvumilivu na subira hadi msimamo mkali na wa maamuzi. Tofauti hizi zilitegemea aina ya upinzani na zilidhihirisha misingi ya uadilifu, kulinda mfumo wa Kiislamu na kuheshimu utu wa binadamu.

Lengo kuu la utawala wa Amirul-Mu’minin (a.s) ni kuwaongoza wanadamu / mpaka kati ya uhuru wa kujieleza na vitendo dhidi ya usalama wa umma


Uainishaji wa wapinzani katika utawala wa Amirul-Mu’minin (a.s)
Nourmofidi aliwagawanya wapinzani wa wakati wa Imam Ali (a.s) katika makundi matatu makuu:
Wapinzani wa kiitikadi (fikra):
Wale waliokuwa na tofauti za kimawazo na Imam lakini hawakuchukua hatua za kisiasa au kiusalama. Imam aliwashughulikia kwa uvumilivu, mazungumzo na kuwashawishi kwa hoja.


Wakosoaji wa kisiasa:
Wale waliokosoa baadhi ya maamuzi ya kisiasa au kiutawala ya Imam. Msimamo wa Imam kwao ulikuwa ni wa busara, maelezo na kuvumilia.
Wapinzani wa kiusalama na waasi:


Makundi yaliyochukua hatua za vitendo, hata za kijeshi, na kuhatarisha usalama wa umma. Imam Ali (a.s) aliwashughulikia kwa msimamo mkali na bila kusita.


Alitoa mfano wa kihistoria wa Khawarij, akieleza kuwa upinzani wao ulianza kama tofauti ya fikra, kisha ukageuka kuwa uasi wa kijeshi katika vita vya Nahrawan. Imam Ali (a.s) hadi dakika za mwisho alijaribu kuwatenganisha watu waliodanganywa na viongozi wao wenye misimamo mikali, na alichukua hatua ya kijeshi tu pale usalama wa umma ulipokuwa hatarini.


Misingi ya mwenendo wa kisiasa wa Amirul-Mu’minin (a.s)
Mhadhiri huyo alitaja misingi mikuu iliyokuwa ikiongoza mwenendo wa Imam Ali (a.s):

1_Uadilifu: Kiini cha utawala wa Alawi; Imam hakuwahi kuacha uadilifu katika hali yoyote.
2_Kulinda mfumo wa Kiislamu: Usalama, utulivu na ustawi wa jamii ni nguzo za msingi za utawala.
3_Kuzingatia maslahi ya umma: Maslahi ya Uislamu na Waislamu yalikuwa mbele ya maslahi binafsi.
4_Kuheshimu utu wa binadamu: Hata kwa wapinzani na maadui, Imam alihifadhi maadili, haki na heshima ya kibinadamu.


Alisisitiza kuwa misingi hii, pamoja na upeo wa kiroho na kimaadili wa Imam Ali (a.s) kama kielelezo cha sifa za Mwenyezi Mungu, inatoa mfano wa utawala unaojengwa juu ya haki, busara na uchaMungu.


Kusimamia upinzani: kutoka uvumilivu hadi msimamo mkali
Nourmofidi alieleza kuwa mwenendo wa Imam Ali (a.s) haukuwa wa upande mmoja au rahisi, bali ulikuwa wa hatua na nyuso nyingi: kuanzia uvumilivu, mazungumzo na nasaha, hadi mapambano ya kijeshi pale ilipolazimu. Alisisitiza kuwa ni kosa kuangalia upande mmoja tu wa mwenendo huo bila kuzingatia lengo kuu, ambalo ni kuwaongoza wanadamu kuelekea kwenye sa‘ada (fanaka) ya kweli.


Mtazamo wa usalama katika dunia ya leo
Akiangazia ulimwengu wa sasa, Nourmofidi alisema kuwa dhana ya “kuchukua hatua dhidi ya usalama wa umma” leo ni pana zaidi kuliko zamani. Vita vya kisasa haviko tu katika uwanja wa kijeshi, bali pia ni:

1_Vita vya fikra na utambuzi,
2_Vita vya mtandaoni (cyber),
3_Na vita vya vyombo vya habari.


Alionya kuwa ni lazima kuwa na ufafanuzi sahihi, wa kitaalamu na usioegemea matakwa binafsi kuhusu usalama wa taifa, ili kuepuka misimamo ya kupindukia au kupuuzia. Kama alivyofanya Imam Ali (a.s) kwa kutofautisha kati ya waliodanganywa na waasisi wakuu wa fitna, ndivyo pia leo inavyopasa kutenganisha wananchi wasio na uelewa na mitandao iliyoratibiwa ya maadui.

Lengo kuu la utawala wa Amirul-Mu’minin (a.s) ni kuwaongoza wanadamu / mpaka kati ya uhuru wa kujieleza na vitendo dhidi ya usalama wa umma


Lengo kuu la utawala wa Amirul-Mu’minin (a.s): kuwaongoza wanadamu
Mwisho, Sayyid Mujtaba Nourmofidi alisema: Lengo kuu la utawala wa Imam Ali (a.s) lilikuwa kuwaongoza wanadamu kuelekea furaha ya kweli na ukaribu na Mwenyezi Mungu, na mienendo yake yote ya kisiasa, kijamii na kitamaduni inaeleweka ndani ya mfumo huu.


Alisisitiza kuwa kusimamia upinzani katika utawala wa Kiislamu kunapaswa kujengwa juu ya misingi hiyo hiyo ya uadilifu, kulinda mfumo, maslahi ya umma na kuheshimu utu wa binadamu.


Alimalizia kwa kusema kuwa katika zama hizi za vitisho vipya na aina mpya za upinzani, mfano wa utawala wa Imam Ali (a.s) unaweza kuwa mwongozo wa vitendo kwa mifumo ya kidini na kimaadili katika kusimamia migogoro, kulinda usalama na wakati huo huo kuhifadhi heshima ya binadamu.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha