Ayatullah Khamenei ameyasema hayo Jumamosi jijini Tehran akihutubia maelfu ya watu kutoka matabaka mbalimbali waliokusanyika katika Huseiniyya ya Imam Khomeini mjini Tehran, kuadhimisha Sikukuu ya Eid al-Mab’ath, siku ya kupewa Utume Nabii Muhammad (SAW) inayosadifiana na tarehe 27 mwezi wa Rajab.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amezungumzia uwezo mkubwa wa Uislamu wa kufanya mabadiliko katika jamii ya mwanadamu wa leo kama yale ya zama za awali za Uislamu na kubadilisha jamii zilizokumbwa na ujinga, ukandamizaji, utumiaji wa mabavu, hofu na kiburi kuwa jamii zinazofurahia haki, uokovu na heshima.
Akilipongeza taifa la Iran, Umma wa Kiislamu na wapigania uhuru wote wa dunia kwa sikukuu hii muhimu zaidi katika historia ya mwanadamu, Imam Khamenei amekutaja kupewa Utume Nabii Muhammad (SAW) kuwa ni siku ya kuzaliwa Qur'ani Tukufu, kuwajulisha wanadamu mafundisho ya Mwenyezi Mungu ya kulea mwanadamu mkamilifu, mwanzo wa ustaarabu wa Kiislamu na siku ambayo bendera ya haki, udugu na usawa ilipandishwa juu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja jamii nyingi za wanadamu za leo, hasa jamii za Magharibi, kuwa zimenasa katika ufisadi mkubwa wa kimaadili, ukandamizaji, dhuluma, uonevu na kiburi, licha ya mwonekano na fasihi zao zinazotofautiana na zile za kipindi cha Ujahilia na akasema: Uislamu na Waislamu wenye imani na itikakdi thabiti wanaweza kuongoza ulimwengu wa leo kutoka kwenye mporomoko wa kuelekea kwenye bonde la ufisadi na uharibifu hadi kwenye vilele vya haki, uokovu na heshima; na kutoka Jahanamu hadi peponi, kwa sharti la kufanya kazi kwa imani ya kina na ya pande zote.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria fitina ya hivi karibuni iliyosababisha maumivu na madhara kwa wananchi na nchi, akisema: Fitina hii imezimwa kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kwa mikono ya taifa, maafisa wa serikali na wanausalama wenye ujuzi, lakini lazima tujue chanzo cha fitina hiyo sababu zake; ni nani waliokuwa sehemu zake, na mienendo yetu kwa adui itakuwaje?
Marekani kuwa ndio chanzo cha fitina
Ayatullah Ali Khamenei ameitaja Marekani kuwa ndio chanzo cha fitina ya hivi karibuni nchini Iran. Akielezea lengo kuu la Wamarekani katika njama mbalimbali amesema: "Lengo na sera endelevu ya Marekani, na si rais wake wa sasa pekee, ni kuimeza Iran na kurejesha utawala wake wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi juu ya nchi yetu; kwa sababu hawawezi kustahamili nchi yenye ukubwa, idadi ya watu, suhula na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, tena katika eneo nyeti la kijiografia."
Imam Khamenei amezitaja kauli za Rais wa Marekani, aliyewaarifisha wahujumu na wauaji kuwa ni "taifa la Iran", kuwa ni tuhuma kubwa dhidi ya taifa hilo na akasema: "Rais wa Marekani aliwahimiza waziwazi wafanya fujo, na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ziliwapa msaada nyuma ya pazia; kwa hivyo, tunamtambua Rais wa Marekani kuwa na hatia, kwa sababu ya mauaji na uharibifu na kwa sababu ya tuhuma alizotoa dhidi ya taifa la Iran."
Akizungumzia vibaraka wa nyanjani, amesema: "Mawakala waliokuwepo maeneo ya machafuko walikuwa wa aina mbili; kundi moja lilichaguliwa kwa uangalifu na mashirika ya ujasusi ya Marekani na Israel, na pamoja na kupewa kiasi kikubwa cha pesa, vilevile walipewa mafunzo kuhusu masuala kama vile jinsi ya kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine, kuchoma moto, kusababisha hofu na kutoroka polisi, na idadi kubwa ya vibaraka hao waovu na wahalifu wamekamatwa kutokana na kazi nzuri ya polisi na vikosi vya usalama."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kundi la pili la mawakala waliokuwa nyanjani ni vijana mabarobaro walioathiriwa na kundi la kwanza, akiongeza kuwa: Kundi hili halikuwa na uhusiano wowote na utawala wa Kizayuni au mashirika ya ujasusi, bali walikuwa watu wasio na uzoefu ambao waliathiriwa na viongozi wa fitina hiyo, na walijihusisha na vitendo na uovu ambao hawakupaswa kufanya kutokana na mihemko.
Hata hivyo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, "katika fitina za hivi karibuni, sifa ya kipekee ilikuwa kwamba Rais wa Marekani mwenyewe aliingilia kati, alitoa matamshi, kuwahamasisha wafanya ghasia na hata alizungumzia kutoa msaada wa kijeshi."
Habari inayohusiana:
Kiongozi Muadhamu: Kujitokeza wananchi katika maandamano ya kitaifa Iran kumevuruga njama za maadui
"Hii ilionyesha wazi kwamba machafuko ya hivi karibuni ni uchochezi uliochochewa na Marekani. Wamarekani walipanga, na kwa kuzingatia uzoefu wa miaka 50, nasema kwa uwazi kwamba lengo la Marekani ni kuimeza Iran," amesisitiza Ayatullah Khamenei.
Akiashiria hatua za kinyama na kikatili kabisa kama vile kuwazingira na kuwachoma moto vijana kadhaa wakiwa hai msikitini au kuua mtoto wa kike wa miaka mitatu na mwanamume na mwanamke asiye na ulinzi wala hatia, ameeleza kuwa: vitendo hivi ni sehemu ya mpango uliotayarishwa awali wa uasi na walikuwa na silaha baridi na pia silaha za moto ambazo ziliingizwa nchini kutoka nje ya nchi na kusambazwa kwa vibaraka wao ili kufanya uhalifu huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, taifa la Iran limevunja mgongo wa fitna na kusema: Taifa la Iran na maandamano yake ya mamilioni ya wananchi tarehe 12 Januari, yameifanya siku hii kuwa ya kihistoria katika kitabu cha rekodi ya matukufu yake mengi na limesambaratisha fitina hiyo kwa kupiga konde kali vinywani mwa maadui.
Ayatullah Khamenei amekutaja kushindwa kwa Marekani kwa mikono ya wananchi wa Iran katika fitina ya sasa kuwa ni mwendelezo wa kushindwa Marekani na Wazayuni katika Vita vya Siku 12 na akasema: Walianzisha fitina hii kwa ajili ya kazi nyingine kubwa zaidi, na bila shaka taifa limezima fitina hiyo, lakini hilo halitoshi, na lazima Marekani iwajibishwe kwa matendo yake.
Your Comment