Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Oktoba 2022

20:57:19
1311389

Mazungumzo ya amani baina ya waasi wa TPLF na serikali ya Ethiopia, yaakhirishwa

Mazungumzo ya amani baina ya waasi wa TPLF na serikali ya Ethiopia ambayo yanasimamiwa na Umoja wa Afrika yameakhirishwa kwa sababu za kilojistiki.

Wanadiplomasia wawili wametangaza habari hiyo leo Ijumaa na kuongeza kuwa, mazungumzo hayo yalikuwa yafanyike mwishoni mwa wiki, lakini yameakhirishwa kwa sababu za kilojistiki ingawa hawakusema yatafanyika lini.

Siku ya Jumatano, pande mbili hasimu, kundi la TPLF na serikali ya Ethiopia zilikubaliana na mpango wa Umoja wa Afrika wa kufanyika mazungumzo ya amani baina yao nchini Afrika Kusini. Mazungumzo hayo yangekuwa ya kwanza rasmi kufanyika baina ya pande hizo tangu zilipoanza kupigana mwezi Novemba 2020.

Mzozo huo umeua maelfu ya raia na kufanya mamilioni ya watu kuwa wakimbizi. Pande zote mbili hapo awali zilisema zimejiandaa kushiriki katika mazungumzo ya upatanishi yanayosimamiwa na AU lakini mapigano makali yameendelea kushuhudiwa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Misaada ya kibinadamu wakipelekewa wakazi wa mji wa Mekelle, makao makuu wa jimbo la Tigray la Ethiopia

 

Redwan Hussein, mshauri wa usalama wa taifa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, alisema kwenye Twitter kwamba: Serikali yetu imekubali mwaliko huu ambao unaambatana na msimamo wetu wa kanuni kuhusu utatuzi wa amani wa mzozo huo na haja ya kuwa na mazungumzo bila ya masharti.

Katika taarifa yao, waasi wa TPLF nao walisema kuwa wamekubali mwaliko huo wa mazungumzo ambayo yalikuwa yamepengwa kuongozwa na mwenyekiti wa kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat.

Serikali ya Ethiopia ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed inawatuhumu waasi wa TPLF kwa wanajaribu kurejesha utawala wao katika nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika. TPLF iliongoza muungano tawala nchini Ethiopia kwa karibu miaka 30 kabla ya kuondolewa madarakani kwenye uchaguzi wa mwaka 2018 ambao ulimuingiza madarakani Abiy Ahmed kwa njia ya demokrasia. TPLF inamtuhumu Abiy Ahmed kuwa amejiongezea madaraka na kuwakandamiza Watigray.

342/