Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

5 Februari 2024

19:15:07
1435510

Kiongozi Muadhamu anawataka wasomi wa Kiislamu kuanzisha matakwa ya umma ya kukata uhusiano na Israel

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, anasema wasomi wa Ulimwengu wa Kiislamu wanabeba dhima nzito kuhusiana na matukio yanayojiri huko Gaza na kwamba wanapaswa kuanzisha matakwa ya umma ya kukata uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo mapema leo katika kikao chake na makamanda na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Iran mjini Tehran.

Kiongozi Muadhamu ametahadharisha kuhusu "maafa ya binadamu" yanayotokea Ukanda wa Gaza kwa himaya na misaada ya Marekani kwa utawala wa Israel na kuongeza kuwa: Shakhsia na watu mashuhuri katika Ulimwengu wa Kiislamu wanapaswa kuhimiza wito kutoa pigo la maangamizi kwa uutawala haramu wa Israel. Amesisitiza kuwa: "Pigo la mwisho halimaanishi kwenda vitani na utawala wa Kizayuni (Israel), lakini lina maana ya kukata uhusiano wa kiuchumi na utawala huo."

Ayatullah Khamenei amesema kuwa mataifa yana uwezo wa kuzishinikiza serikali za nchi zao kukomesha himaya na uungaji mkono wao kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Amesema: Ingawa utawala huu katili na wenye sifa kama za mbwa mwitu umechukua maisha ya wanawake, watoto na wagonjwa na kuua zaidi ya watu 20,000, baadhi ya nchi za Kiislamu bado zinaupatia misaada ya kiuchumi na hata silaha.

Kiongozi Muadhamu ameonya kuhusu "njama mahsusi" za adui dhidi ya wasomi na shakshia wa Iran ndani na nje ya nchi, akisema adui kimsingi anataka kuzuia mchango mkubwa wa wasomi nchini na kuibua shaka miongoni mwao.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, nguvu za taifa huimarisha usalama wa taifa na kusema kwamba, njama za adui zitazimwa pale atakaposhuhudia uwepo na utayarifu wa watu wa Iran pamoja na nguvu ya utawala wa Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, uongozi, sera na zana za kijeshi za Jeshi la Anga vilikuwa chini ya udhibiti kamili wa Marekani; Hata hivyo, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, waumini na wanamapinduzi katika jeshi la anga walianzisha jihadi ya kijitosheleza na kuliondoa jeshi hilo katika udhibiti wa Marekani.

Kiongozi Muadhamu pia amepongeza ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran katika maandamano ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyouangusha utawala wa Pahlavi uliokuwa ukisaidiwa na kuungwa mkono na Marekani.Ayatullah Khamenei amesema ana matumai kwamba, Wairani watashiriki kwa wingi pia katika maandamano ya mwaka huu ya Februari 11, ambayo yanaashiria nguvu kubwa ya taifa.

342/