10 Agosti 2019 - 10:00
Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji: Muamala wa Karne utasambaratika kwa hima na imani ya mrengo w

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa wito kwa mataifa ya Waislamu kuungana kukabiliana na njama za maadui huku akikisitiza kuwa 'Muamala wa Karne' kuhusu kadhia ya Palestina utafeli kwa hima na imani ya mrengo wa muqawama.

(ABNA24.com) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa wito kwa mataifa ya Waislamu kuungana kukabiliana na njama za maadui huku akikisitiza kuwa 'Muamala wa Karne' kuhusu kadhia ya Palestina utafeli kwa hima na imani ya mrengo wa muqawama.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo katika ujumbe uliotangazwa leo Jumamosi kwa Mahujaji wa Baitullahi Al Haram ambapo amesisitiza kuwa, dhulma kubwa zaidi katika karne za karibuni imejiri huko Palestina. Ameongeza kuwa, kadhia muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu ni kadhia ya Palestina ambayo ni ya kwanza katika kadhia zote za kisiasa za Waislamu wa madhehebu, rangi na lugha zote.

Ayatullah Khamenei ameendelea kusema kuwa, Hadaa ya 'Muamala wa Karne' ambayo inaandaliwa na dola dhalimu la Marekani pamoja na wahaini wanaoandamana naye, ni jinai ambayo si dhidi ya haki ya taifa la Palestina pekee bali pia ni dhidi ya jamii nzima ya wanadamu. Ameongeza kuwa, kwa Taufiki yake Mwenyezi Mungu, Taifa la Palestina halijakubali kushindwa na wala halikukaa kuwa mtazamaji na hivyo leo limejitokeza kwa ushujaa zaidi katika medani zaidi ya siku za nyuma; lakini ili mafanikio yapatikane kunahitajika msaada wa Waislamu wote.

Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa, amali ya kujibari na kujiweka mbali na mushirikina maana yake ni kuchukizwa na kila aina ya uonevu, udhalimu, ubaya, ufisadi wa mataghuti wa zama zote.

Aidha amesema leo kujiweka mbali na mrengo wa shirki na kufri, ambao ni mrengo wa mustakbirina, kinara wake akiwa ni Marekani, kuna maana ya kujiweka mbali na mauaji yanayotekelezwa dhidi ya wanaodhulumiwa na pia kuna maana ya kujiweka mbali na uenezaji vita; kuna maana ya kulaani vitovu vya ugaidi kama ule ugaidi  wa Daesh (ISIS) na Blackwater ya Marekani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake kwa Mahujaji ameendelea kusema kuwa, kujibari na mushirikina pia kuna maana ya  kuchukizwa na ubaguzi kwa msingi wa jiografia, kaumu au rangi ya ngozi. Hali kadhalika, amesema kujibari na mushirikina kuna maana ya kuchukizwa na tabia za kiistikbari na khabithi za  madola makubwa vamizi na fitina zinazotekelezwa dhidi ya wale wenye uungwana na uadilifu ambao Uislamu unataka wote wafuate.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, wasomi wa Ulimwengu wa Kiislamu, ambao baadhi yao kutoka nchi mbali mbali hivi sasa wanashiriki katika Hija, wana jukumu nzito na muhimu katika mabega yao.

Kiongozi Muadhamu amesema wasomi wanapaswa kufanya hima na kutumia ubunifu kufikisha haya mafunzo kwa mataifa na fikra za umma ili waweze kuibua mabadilishano ya kimaanawi ya fikra na pia mabadilishano ya motisha, uzoefu na ujuzi.

/129