Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Algeria imeeleza kuwa, hatua ya waziri huyo mzayuni mwenye misimamo mikali na ya chuki ni kinyume cha sheria na kwamba, inakariri wazi na bayana ukiukaji wa sheria na maazimio ya kimataifa.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imelaani hujuma zilizoratibiwa za kuvamia msikiti wa al-Aqswa na kufanya vitendo vya kichochezi na kujeruhi hisia za Waislamu na Wapalestina.
Algeria imeitaka pia jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ipasavyo mbele ya hujuma na mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Itamar Ben-Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni,Jumapili ya juzi asubuhi alivamia katika Msikiti wa Al-Aqswa ikiwa ni mara ya pili tangu achukue wadhifa kama waziri wa usalama wa ndani wa Israel.
Hujuma hiyo ya uvamizi ilitekelezwa kwa kuungwa mkono pakubwa na wanajeshi wa Kizayuni; ambapo Be-Gvir baada ya kupita katika maeneo tofauti ya Msikiti wa Al-Aqsa, aliekekea katika eneo la ukuta wa Buraq (mahali ambapo hafla za kidini za Wazayuni hufanyika).
Msikiti wa Al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho muhimu wa Kiislamu na Palestina mjini Beitul Muqaddas na utawala wa Israel unajaribu kuharibu umuhimu huo, lakini kusimama kidete na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala wa Kizayuni na kuufanya ushindwe kufikia malengo yake maovu dhidi ya Waarabu na Waislamu.
342/