Akihutubia Chatham House siku ya Jumatano katika sehemu ya ziara yake rasmi nchini Uingereza, Jaishankar alibainisha kwamba hakuna mwafaka uliofikiwa katika BRICS, ambayo sasa imepanuliwa, kuhusu suala la sarafu ya Marekani kuhodhi na kutawala biashara ya kimataifa, jambo ambalo wanachama wengi wa BRICS wanalipinga waziwazi.
"Aidha, nieleze kwa udhati kabisa kwamba, sidhani kama kuna msimamo wa pamoja wa BRICS juu ya hili. Nadhani wanachama wa BRICS, na kwa kuwa sasa tuna wanachama wengi zaidi, wana misimamo tofauti sana kuhusu suala hili. Kwa hiyo, pendekezo au dhana kwamba mahali fulani kuna msimamo wa umoja wa BRICS dhidi ya dola, nadhani, halijathibitishwa na ukweli,” alibainisha waziri huyo.
Alipoulizwa kama India nayo inataka kupanua satua ya sarafu yake ya rupia duniani na hivyo kukabiliana na dola ya Marekani, Jaishankar alikana haraka dai hilo na kusema: "hatujawahi kuwa na tatizo na dola. Uhusiano wetu na Marekani pengine ni mzuri zaidi wakati huu kuliko ilivyowahi kuwa. Hivyo hatuna nia kabisa ya kuihujumu dola hata kidogo”.
Waziri wa Mambo ya Nje wa India ametoa matamshi hayo wiki kadhaa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kudai kwamba BRICS "inajaribu kuivuruga sarafu ya dola ya Marekani" na kwamba kundi hilo "limekufa" kufuatia vitisho alivyotoa vya kutoza ushuru wa 150% kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi wanachama wa BRICS.
BRICS iliundwa na Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini na imepanuka katika miaka miwili iliyopita na kujumuisha Misri, Ethiopia, Iran, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) na Indonesia. Saudi Arabia imekubali uanachama lakini bado haijajiunga rasmi.../
342/
Your Comment