Akizungumza pambizoni mwa mkutano wa kila mwaka wa Bunge la China jana Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje, Wang Yi aliikosoa Washington kwa kuiwekea 'ushuru wa adhabu' licha ya Beijing kuchukua hatua kama mshirika wa kutegemewa wa kimataifa na kusaidia kukabiliana na mgogoro wa mihadarati aina ya fentanyl unaoisakama Marekani.
"Ikiwa upande mmoja unatoa mashinikizo kwa upofu, China itapinga hilo kwa uthabiti," Wang ameonya na kuongeza kuwa, "Hakuna nchi inayoweza kufikiria kuwa inaweza kukandamiza China kwa upande mmoja huku ikiendeleza uhusiano mzuri na China kwa upande mwingine."
Tangu Trump aingie madarakani, Marekani imeongeza maradufu ushuru kwa bidhaa zote za China, kutoka asilimia 10 hadi 20, na kutonesha kidonda cha ushuru uliokuwepo kwa maelfu ya bidhaa za China.
Mwezi uliopita, Rais wa Marekani pia aliamuru ushuru mpya kwa bidhaa kutoka China, Mexico, na Canada, akitaja haja ya kulinda maslahi ya Marekani na kuashiria wasiwasi juu ya usawa wa biashara, uhamiaji haramu, na utitiri wa dawa za kulevya nchini Marekani.
Serikali ya China imejibu mapigo kwa kuongeza ushuru wa kuanzia 10% hadi 15% kwa bidhaa mbalimbali za Marekani, ikiwa ni pamoja na mazao ya kilimo na bidhaa za nishati.
342/
Your Comment