Katika siku ya 48 ya kampeni kubwa ya jeshi la utawala wa Kizayuni kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, mashambulizi ya wazayuni katika maeneo mbalimbali ya eneo hilo yangali yanaendelea, na wavamizi hao wangali wanaendelea kuzingira kambi za kaskazini mwa Ukingo huo. Waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Yisrael Katz ameviamuru vikosi vya jeshi la utawala huo ghasibu viendelee kuziwekea mzingiro kambi za wakimbizi wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi, kwa uchache hadi mwisho wa mwaka huu. Duru za ndani katika kambi ya Nur Shams iliyoko Tulkarm huko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi zimeripoti kuwa utawala ghasibu wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi yake ya kijeshi kwenye kambi hiyo na umesababisha uharibifu mkubwa kwa kubomoa nyumba na majengo ya eneo hilo. Wazayuni wamewatimua makumi ya maelfu ya wakazi wa kambi ya Nur Shams na wametoa onyo tena kwa wakazi wa nyumba kadhaa la kuwataka wazihame nyumba zao.
Philippe Lazzarini, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amelaani hatua ya utawala wa Kizayuni ya kubomoa nyumba chungu nzima katika Ukingo wa Magharibi na akabainisha kwamba, hatua hizo zimekuwa na taathira kubwa za madhara na uharibifu kwa maisha ya maelfu ya Wapalestina. Lazzarini ameandika kwenye ukurasa wake binafsi kwenye mtandao wa kijamii wa X: "kambi za wakimbizi za Jenin, Tulkarm na Nur Shams takribani zimebaki tupu bila wakazi wake Wapalestina, huku miundomsingi mingi ya kiraia, zikiwemo nyumba ikiendelea kuharibiwa na kubomolewa. Sasa hivi watu wanakabiliana na ukweli kwamba hawana mahali pa kurudia tena".
Abdul Rahman Shadid, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuhusiana na hujuma zinazofanywa na Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi kwamba, kwa operesheni zake ubomoaji na kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa mikoa ya Ukingo wa Magharibi, utawala wa Kizayuni umedhamiria kuhitimisha na kulifuta kikamilifu suala la wakimbizi.
Kamanda huyo wa Hamas amesema, Wazayuni wanaendelea kubomoa nyumba za watu katika kambi za Jenin, Tulkarm, na Nur Shams na akabainisha kuwa, lengo la Israel la kufanya vitendo hivyo vya jinai ni kutaka kuufuta Muqawama na dhamira yake ni kupanua wigo wa operesheni hizo hadi kwenye kambi nyingine zilizoko Ukingo wa Magharibi.
Muqawama wa Kiislamu wa Palestina umesisitiza kwamba, wananchi wa Palestina inapasa wasimame imara kukabiliana na mashambulizi hayo na umebainisha kuwa, kuna ulazima wa kuzidishwa Muqawama wa kukabiliana na Israel na walowezi wa Kizayuni, na kwamba hata inchi moja ya ardhi ya Palestina isibaki kuwa mahapa penye amani na salama kwa wazayuni maghasibu.
Mashambulizi ya utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya majengo ya makazi, ya tiba, ya elimu na ya kidini katika Ukingo wa Magharibi yanafanywa chini ya kivuli cha uungaji mkono mkubwa wa Marekani na kimya na ulegevu wa kutochukua hatua yoyote unaoonyeshwa na nchi za Ulaya zinazojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Umoja wa Ulaya umetosheka tu na kuutaka utawala wa Kizayuni uheshimu sheria za kimataifa, uwalinde raia katika operesheni zake za kijeshi, na uwaruhusu wakimbizi warejee kwa usalama kwenye makazi yao. Ukweli ni kwamba, serikali za nchi Ulaya hazilaani suala la msingi, yaani mashambulizi ya Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi, bali unawataka Wazayuni hao wahakikishe usalama tu wa raia wa Ukingo wa Magharibi, ilhali hakuna vikosi vya kijeshi katika eneo hilo ghairi ya Muqawama wa wananchi wa kukabiliana na uvamizi na uchokozi wa Wazayuni.
Wakati huo huo, kuna watu ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel wanaobainisha kwa uwazi zaidi malengo ya utawala wa Kizayuni ya kuishambulia Ghaza na Ukingo wa Magharibi. Mmoja wa watu hao ni Gideon Levi, mwandishi wa gazeti la Haaretz. Katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti hilo lenye mielekeo ya mrengo wa kushoto, Levi ameandika: "Ukingo wa Magharibi pamoja na Ghaza, zinaunda maeneo ya Palestina. Hata kama kidhahiri, eneo la Ukingo wa Magharibi liko chini ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, lakini Israel inaendelea kudhibiti maisha na vifo vya wakazi wake".
Kuhusiana na namna utawala huo unavyoshirikiana na walowezi wa Kizayuni, Gideon Levy anasema: “wanataka kuendesha vita kamili katika Ukingo wa Magharibi; vita ambavyo vitawawezesha kutekeleza mpango wao mkubwa wa kuwatimua kwa wingi Wapalestina. Katika hali ya kutisha, huu ndio mpango pekee ilionao Israel kwa ajili ya kutatua kadhia ya Palestina". Kwa anavyoeleza mchambuzi huyo Muisrael, mashambulizi ya kikatili wanayofanya Waisraeli dhidi ya watu wa Ukingo wa Magharibi yanaweza yakawa sababu ya kuibuka Intifadha nyingine mpya, yaani uasi wa umma, ya Wapalestina.../
342/
Your Comment