Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA – Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Reza Aref, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nyanja za kiutawala na kijamii, akisema Serikali ya Iran imeridhishwa sana na kiwango cha ushiriki wao na kwamba utendaji wao katika majukumu waliyopewa umekuwa wa kipekee.
Aref aliyasema hayo katika kikao cha kwanza cha Baraza la Kitaifa la Wanawake na Familia, ambapo alieleza umuhimu mkubwa wa nafasi ya wanawake na familia katika jamii ya Iran.
Alisisitiza haja ya kuzingatia haki za wanawake na kuimarisha nafasi yao katika jamii, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini Iran ni wanawake.
Kwa mujibu wa Aref, Iran inahitaji kutumia ipasavyo uwezo na vipaji vya wasomi na wataalamu wanawake na wanaume ili kufikia malengo ya taifa na kuendeleza maendeleo ya nchi.
Umuhimu wa Mama katika Familia
Akizungumzia nafasi ya umama katika utamaduni wa Kiislamu na Iran, Aref alisema hakuna nafasi inayoweza kufikiriwa kuwa muhimu zaidi kuliko umama, akisisitiza kuwa umuhimu wake hauwezi kulinganishwa na jambo lingine.
Aidha, alieleza kuwa wanawake wana nafasi ya juu katika mafundisho na kauli za viongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akirejea msisitizo wa Imam Ruhullah Khomeini (r.a.) kuhusu heshima na hadhi ya mwanamke.
Aref alisema hata katika kilele cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, Imam Khomeini (r.a.), kupitia mahojiano yake na vyombo vya habari vya Magharibi akiwa Paris, alisisitiza kwa namna ya pekee nafasi na hadhi ya wanawake.
Wanawake Washiriki katika Nyanja Mbalimbali
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais pia amepongeza nafasi inayotekelezwa na wanawake kwa wakati mmoja katika familia na katika shughuli za kijamii.
Alisema kuwa wasichana na wanawake wa Iran kwa sasa wanashiriki kikamilifu katika nyanja mbalimbali za maisha ya taifa, zikiwemo sayansi na teknolojia.
Aref alieleza kuwa vita vya hivi karibuni vimekuwa kwa kiasi kikubwa vita vya sayansi na teknolojia, akisema kwa furaha kuwa wanasayansi wanawake vijana wa Iran nao wameonyesha uwezo mkubwa katika nyanja hizo.
Wanawake katika Kukabiliana na Vita vya Kiuchumi
Aref pia alisisitiza umuhimu wa nafasi ya wanawake katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kulinda mshikamano wa kijamii nchini Iran.
Alisema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kile alichokiita “Jabhatu ya Mtaa”, katika kipindi cha siku 200 zilizopita, akisisitiza kuwa mchango wao katika jamii haupaswi kupuuzwa.
Aidha, alitoa wito wa kufanyiwa marekebisho baadhi ya sheria zinazohusiana na wanawake, pamoja na kuendelezwa kwa mchakato ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya 14 katika eneo hilo.
Mpango wa Ajira na Uwezeshaji Kiuchumi
Mwisho wa kikao hicho, ilikubaliwa kuunda kikosi kazi kitakachokusanya maoni ya wajumbe wa Baraza la Kitaifa la Wanawake na Familia kuhusu mpango wa ajira na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi unaozingatia familia.
Mapendekezo hayo yatajadiliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Ushirikiano, Kazi na Ustawi wa Jamii, pamoja na Shirika la Mipango na Bajeti, kabla ya kuandaliwa kwa waraka wa utekelezaji wa mpango huo ndani ya mamlaka ya Serikali.
Maoni yako