29 Septemba 2026 - 23:12
Je, Mtoto Wako Anaogopa Zaidi Hatari za Intaneti au Mwitikio Wako (Radiamali Yako)??

Ripoti za kimataifa zinaonyesha kuwa madhara ya mazingira ya mtandaoni kwa watoto ni makubwa na ya kina. Hata hivyo, tatizo kubwa zaidi hutokea pale mtoto anapoficha madhara aliyoyapata kwa sababu ya kuogopa mwitikio wa wazazi; ilhali nyumbani panapaswa kuwa mahali salama zaidi ambapo mtoto anaweza kueleza hata ukweli mchungu zaidi.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hussein Amin, mwandishi na mtafiti wa dini, katika makala maalumu kwa ABNA, amezungumzia moja ya changamoto muhimu sana zinazozikabili familia za leo, nayo ni namna watoto wanavyokabiliana na simu za mkononi na kuingia katika ulimwengu mpana na bahari isiyo na mipaka ya anga ya mtandao.

Je, Mtoto Wako Anaogopa Zaidi Hatari za Intaneti au Mwitikio Wako (Radiamali Yako)??

Muhammad Hussein Amin / Mwandishi na Mtafiti wa Dini

Katika zama ambazo watoto wetu wanaingia katika ulimwengu usio na mipaka wa intaneti kabla hata ya kuufahamu kikamilifu ulimwengu halisi, swali lenye uchungu na la msingi ni hili: Ikiwa mtoto wetu asiye na hatia atateleza katika mazingira haya yenye changamoto nyingi au akatumiwa vibaya, je, nyumbani bado ni mahali salama kiasi cha kumfanya amweleze mzazi wake siri yake nzito, au kwa hofu ya “mahakama ya nyumbani” ataamua kunyamaza mbele ya mbwa mwitu wa mtandaoni?

Wakati Nyumba Inapogeuka Kutoka Mahali pa Kimbilio Kuwa Mahakama

Takwimu na uchambuzi mbalimbali unaotambulika kimataifa, miongoni mwao ripoti rasmi za UNICEF [1], zinafunua ukweli wa kutisha: wigo wa madhara ya mtandaoni kwa watoto ni mpana sana, lakini sehemu ya madhara ambayo hayaripotiwi kamwe na kubaki ndani ya mioyo ya watoto ni kubwa zaidi na yenye kutisha. Mamilioni ya watoto duniani kote hukumbana na tabia zisizotakiwa, unyanyasaji wa mtandaoni au kuona maudhui yasiyofaa, lakini kwa kuogopa madhara yanayoweza kutokea, hawasemi chochote. Ukimya huu mzito ni ishara ya wazi ya mgogoro wa kihisia; mgogoro ambao kuta za nyumba zimeshindwa kumpatia mtoto kiwango kinachohitajika cha usalama wa kisaikolojia.

Tukichunguza kwa makini tabia za watoto wetu, sababu ya kuficha mambo haya huwa wazi kabisa: mtoto anaogopa zaidi mwitikio wetu wa hasira kuliko hatari yenyewe ya anga ya mtandao! Mtoto anapojua kwamba kukiri kosa la mtandaoni au kueleza tukio chungu alilolipitia kunaweza kumaanisha kutazamwa kwa lawama, kukataliwa, kufokewa na hatimaye kunyang’anywa kabisa vifaa vya kidijitali, hupendelea kubeba mzigo mzito wa hofu hiyo akiwa peke yake. Bila kukusudia, tumegeuza mikono ya familia, ambayo ilipaswa kuwa kitovu cha utulivu, kuwa “mahakama isiyo na huruma” ambamo mtoto anahukumiwa na kuadhibiwa kabla hata ya kusikilizwa kuhusu maumivu yake.

Hali hii ni kinyume na utamaduni halisi wa Kiislamu, ambapo nyumba ni mahali pa utulivu na kimbilio. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Qur’ani Tukufu:

«وَاللَّهُ جَعَلَ لَکُمْ مِنْ بُیُوتِکُمْ سَکَنًا» [2]

(Na Mwenyezi Mungu amewafanyia nyumba zenu kuwa mahali pa utulivu na makazi).

Nyumba ambayo mtoto hana ujasiri wa kusema ukweli kwa sababu ya kuogopa kuhukumiwa na kulaumiwa, imejitenga na ukweli huu wa Qur’ani. Nyumba inapaswa kuwa mahali salama kiasi kwamba mtoto, hata katika nyakati zenye giza zaidi za maisha yake na baada ya makosa yake makubwa zaidi, awe na yakini kwamba mahali pa kwanza na salama zaidi anapoweza kukimbilia ni mikononi mwa baba na mama yake.

Mstari Mwembamba Kati ya “Haya Halisi” na “Hofu Inayopooza”

Moja ya makosa yanayojirudia katika njia yetu ya malezi ya kidini ni kuchanganya kati ya “haya” na “hofu”. Haya ni fadhila ya thamani ya ndani na nuru inayomzuia mwanadamu, kwa heshima na utu, kufanya mambo ya upotovu; lakini ikiwa mtoto wetu anaficha tatizo lake kwa sababu ya kuogopa kuadhibiwa au kuaibishwa, hii si haya, bali ni hofu yenye kuharibu ambayo inalemaza roho yake. Haya katika malezi maana yake ni kuhifadhi mipaka na kuheshimiana, si kujenga ukuta wa hofu kati ya wazazi na mtoto kiasi kwamba njia za mawasiliano na mazungumzo ya kweli zinaharibiwa kabisa.

Ili kuangusha ukuta huu wa hofu, mwenendo wa Ahlul-Bayt (as) unaonyesha njia bora kupitia “ukaribu na kuingia katika kiwango cha mtoto”. Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w.), ambaye alikuwa kitovu cha akili na hekima ya Mwenyezi Mungu, alipokutana na watoto alikuwa akibadilisha mwenendo wake kulingana na ulimwengu wao, na kusema:

«مَنْ کَانَ عِنْدَهُ صَبِیٌّ فَلْیَتَصَابَ لَهُ» [3]

(Mwenye kuwa na mtoto, basi na awe na mwenendo wa kitoto pamoja naye).

Huruma hii na kuingia katika ulimwengu wa mtoto hujenga uaminifu na kumfanya mtoto awaone wazazi wake kuwa watu wa kushirikiana nao siri na marafiki, si maafisa wa kumhoji!

Kwa sababu hiyo, mtazamo wenye athari zaidi katika vyombo vya habari na malezi kwa jamii ya leo ni kuwafundisha watoto wetu kwamba: “Mtoto anapaswa kuogopa hatari ya intaneti, si kuogopa kumweleza baba au mama kuhusu hatari hiyo!” Ikiwa tutaweza kuimarisha imani hii ndani ya mtoto, mara tu atakapokutana na tishio lolote, usumbufu au maudhui yasiyofaa katika anga ya mtandao, badala ya kuficha jambo na kuzama zaidi katika hatari, atawasiliana mara moja na wazazi wake kwa utulivu na kujilinda ndani ya ngome imara ya familia.

Mikono Iliyofunguka Kabla ya Lawama; Mwenendo wa Ahlul-Bayt Katika Kukabiliana na Kosa la Mtoto

Wakati ule mgumu unapofika na mtoto anapofunua kwa uso wenye wasiwasi na sauti inayotetemeka kuhusu tukio chungu au kosa alilolifanya katika anga ya mtandao, namna wazazi watakavyoitikia kwa mara ya kwanza ndiyo inayoweza kuathiri malezi yake. Katika wakati huu nyeti, kabla ya kujilaumu mwenyewe au kumkemea mtoto, fanya jambo moja tu: mkumbatie kwa upendo na ukaribu. Mtoto wako katika hali hii si mhalifu anayehitaji kuadhibiwa, bali ni mtu aliyedhurika ambaye ameponyoka kutoka kwa watekaji wa anga ya mtandao na kukimbilia kwako.

Katika mafundisho yenye thamani ya Shia, kumpenda na kumhurumia mtoto kunachukuliwa kuwa sharti la kujenga jamii yenye afya. Imam Sadiq (a.s.) anasimulia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.):

«أَحِبُّوا الصِّبْیَانَ وَارْحَمُوهُمْ» [4]

(Wapendeni watoto na wahurumieni).

Huruma katika wakati wa mtoto kukiri kosa ni somo kubwa zaidi linalomfundisha kwamba nyumbani si mahali pa kukata tamaa. Mtoto anapoona kwamba uaminifu na ukweli wake umejibiwa kwa upendo na kukubalika, heshima yake binafsi hurejeshwa na hamu ya kurekebisha kosa huamka ndani yake.

Kulinda heshima, kutunza siri na kuhifadhi utu wa mtoto ni msingi usiobadilika katika malezi ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ni “Sattarul-Uyub”, Mwenye Kuficha Aibu, na pia anawahimiza waja Wake kuzificha aibu. Imam Sajjad (a.s.) katika Risalatul-Huquq anasema:

«وَأَمَّا حَقُّ وَلَدِکَ فَتَعْلَمَ أَنَّهُ مِنْکَ... وَأَنَّکَ مَسْئُولٌ عَمَّا وُلِیتَهُ مِنْ حُسْنِ الْأَدَبِ» [5]

(Ama haki ya mtoto wako ni kwamba ujue kuwa yeye anatokana nawe... na kwamba wewe utawajibishwa kuhusu malezi mema na uongozi uliokabidhiwa).

Malezi mema hayapatikani kamwe kwa kujenga hofu na kuvunja heshima; bali hupatikana kwa kujenga mazingira yaliyojaa usalama na ukaribu, ili nyumba daima ibaki kuwa mwanga angavu zaidi wa matumaini kwa mtoto wakati wa dhoruba za anga ya mtandao.

Vyanzo na Maelezo ya Chini ya Ukurasa:

[1] Inarejelea ripoti mbalimbali za uchambuzi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kuhusu usalama wa kidijitali wa watoto na kiwango kikubwa cha unyanyasaji na hatari za mtandaoni ambazo haziripotiwi kutokana na hofu ya watoto kwa wazazi wao.

[2] Qur’ani Tukufu, Sura An-Nahl, Aya ya 80.

[3] Ibn Babawayh (Sheikh Saduq), Muhammad bin Ali, Man La Yahdhuruhul-Faqih, Qom: Daftar Intisharat Islami, chapa ya pili, 1413 H, Juzuu ya 3, uk. 483, Hadithi ya 4707.

[4] Kulayni, Muhammad bin Ya’qub, Al-Kafi, Tehran: Darul-Kutub al-Islamiyyah, chapa ya nne, 1407 H, Juzuu ya 6, uk. 49, Hadithi ya 3. (Matini kamili ya riwaya: «عَنْ أَبِی عَبْدِ اللَّهِ (ع) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (ص): أَحِبُّوا الصِّبْیَانَ وَارْحَمُوهُمْ...»).

[5] Ibn Shu’bah al-Harrani, Hasan bin Ali, Tuhaf al-Uqul ‘an Aal al-Rasul (s.a.w.w.), Qom: Jamiatul-Mudarrisin, chapa ya pili, 1404 H, uk. 263 (sehemu ya Risalatul-Huquq ya Imam Sajjad (a.s.)).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha