Maandamano yanaendelea kwa wiki kadhaa sasa huko Zarzis, mji ambao unaunganishwa na Djerba kwa daraja refu, kufuatia vifo vya watu wa eneo hilo katika ajali za meli za wahamiaji.
Rais wa Tunisia Kais Saied Jumamosi alimkaribisha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na viongozi wengine mjini Djerba baada ya mawaziri wao wa mambo ya nje kukutana katika kisiwa hicho Ijumaa.
"Tulitaka kuandamana na kutoa sauti zetu huko Djerba, lakini majibu ya mamlaka yalikuwa ya kutumia nguvu na tulikandamizwa," Salim Zuraidat, mmoja wa waandamanaji amesema.
Zuraidat ni mmoja wa jamaa za watu kutoka eneo la Zarzis ambao walikufa maji wiki kadhaa zilizopita katika mojawapo ya ajali nyingi za meli za wahamiaji waliokuwa wanapanga kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya.
Walianza kuandamana mjini Zarzis kwa kile walichokiona kuwa ni hatua ya serikali ya kupuuza maafa hayo ikiwa ni pamoja na kushindwa kupeleka boti kutafuta miili ya walioangamia katika ajali.
Maandamano yamekuwa yakifanyika mara kwa mara nchini Tunisia kupinga hatua ya Rais Kais Saied kuchukua madaraka kamili mwaka jana. Waandamanaji pia wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa chakula, mafuta na uingiliaji wa madola ya kigeni hasa Ufaransa katika mambo ya ndani ya nchi hiyo.
342/