13 Mei 2023 - 11:25
Ripoti: Idadi ya wakimbizi duniani ilifikia watu milioni 71 mwaka 2022

Ripoti iliyotolewa na kituo cha kufuatilia waliohama makazi yao, cha Baraza la Wakimbizi la Norway inasema kuwa mwaka 2022, idadi ya wakimbizi wa ndani kote duniani iliongezeka na kufikia milioni 71.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, idadi hiyo imechangiwa pakubwa na vita nchini Ukraine, ambapo kufikia mwishoni mwa mwaka jana, watu milioni 5.9 walifanywa kuwa wakimbizi wa ndani kwa sababu ya vita, ongezeko hili likiwa ni asilimia 20 tangu mwaka 2021.

Katibu Mkuu wa baraza hilo la wakimbizi la Norway, Jan Egeland, amesema migogoro na majanga ya asili mwaka 2022, yalichangia watu kuyahama makwao kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Migogoro na majanga ya kimaumbile pia yalichangia kuongezeka idadi hii, haswa mafuriko na njaa na kufanya idadi ya watu ambao ni wakimbizi nchini kuwa milioni 8.7.

Ripoti ya kituo hicho imetaja mabadiliko ya tabianchi kususan elnino, ambayo yaliendelea kwa mwaka wa tatu mfululizo mwaka jana, kama sababu kuu ya watu kulazimika kuyahama makazi yao, mafuriko nchini Pakistan, Nigeria na Brazili yakichangia hali hiyo.

Ukame mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Somalia, Kenya na Ethiopia, nao uliripotiwa kuchangia kuongezeka idadi ya wakimbizi duniani.

Ni wiki hii tu ambapo shirika la kimataifa la uhamiaji, lilisema kuwa watu laki saba wamefanywa wakimbizi wa ndani kutokana na mapigano yanayoendelea nchini Sudan kati ya jenerali wa jeshi na mkuu wa kikosi cha usaidizi wa haraka ambapo kila siku idadi ya wakimbizi nchini humo na katika nchi jirani inazidi kuongezeka.

342/