13 Mei 2023 - 11:30
UN yakaribisha ahadi ya kulindwa usalama wa raia kutoka kwa makundi hasimu ya Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amekaribisha hatua ya makundi hasimu ya kutia saini makubaliano ya kulindwa usalama wa raia na kuruhusiwa ufikishaji misaada ya kibinadamu nchini Sudan.

Stephane Dujarric, msemaji mkuu wa Guterres amesema na kuongeza kuwa: "Katibu Mkuu (wa Umoja wa Mataifa) anakaribisha kutiwa saini na pande zinazozozana nchini Sudan, azimio la kujitolea kulinda usalama wa raia na kuhakikisha misaada ya kibinadamu wanafikishiwa walengwa kwa usalama kamili."

Aidha amesema: "Wakati wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, hasa wafanyakazi wa ndani ya Sudan, wameendelea kufanya kazi zao katika mazingira magumu sana, Katibu Mkuu ana matumaini kwamba, tamko lake hili litahakikisha kuwa operesheni ya misaada inaongezeka haraka na kwa usalama ili kukidhi mahitaji ya mamilioni ya watu wenye shida nchini Sudan." 

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitizia pia mwito wake wa kusitishwa mapigano mara moja na kutanua wigo wa majadiliano ili kufikia usitishaji vita wa kudumu.

Baada ya takriban wiki moja ya mazungumzo katika mji wa bandari wa Jeddah huko Saudia, jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka, juzi Alkhamisi vilitiliana saini tamko la ahadi ya kulinda usalama wa raia.Msemaji wa Umoja wa Mataifa pia amesema, umoja huo hautaacha kufanya juhudi zozote za kusaidia utekelezaji wa vipengee vya tamko hilo na utaendelea kutoa misaada ya kibinadamu, ni sawa tu mapigano yatasimamishwa au la.

342/