Gavana wa mkoa wa Boucle du Mouhoun magharibi mwa Burkina Faso ametangaza kuwa magaidi walikishambulia kijiji cha Youlou katika wilaya ya Tcheriba na kuuwa raia 33.
Mwezi uliopita pia kijiji kimoja kaskazini mwa Burkina Faso kilikumbwa na jinai sawa na hii ambapo watu 147 waliuliwa. Magaidi hao wenye silaha pia hivi karibuni waliwaua raia 44 katika mashambulizi mawili waliyofanya kaskazini mwa Burkina Faso. Mikoa ya kaskazini mwa Burkina Faso ni kitovu cha shughuli za makundi ya kigaidi na kihalifu yanayofanya mauaji na uporaji mara kwa mara.
Wanamgambo wenye silaha wanadhibiti asilimia 40 ya ardhi nzima ya Burkina Faso. Makundi yenye silaha yanatega mabomu barabarani, yanazingira miji na kuharibu miundombinu ya maji na hivyo kudhoofisha juhudi za kudhamini usalama katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Tokea mwaka 2015, Burkina Faso sawa kabisa na majirani zake Niger na Mali, imeathiriwa na mashambulizi na mauaji yanayofanywa na mamluki wenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al Qaida na Daesh; na kupelekea vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya wakimbizi wengine karibu milioni mbili.
342/