Hayo yamesemwa na meneja mkuu wa ofisi ya Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO mjini Ituri, Marc Karna Soro, ambaye alikuwa akiwahutubia waandishi wa habari katika mji wa Bunia.
Soro, ambaye alikuwa amerejea kutoka kusini mwa eneo la Irumu, alizungumzia hali ya usalama kwa ujumla katika jimbo hilo. Amesema kuwa watu 530 waliuawa katika muda wa miezi miwili na zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao wamejilimbikizia katika vituo mbalimbali vya MONUSCO.
Mikoa ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni pamoja na Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kwa muda mrefu yamekumbwa na mashambulizi ya makundi yenye silaha ambayo yanaua raia na kupora mali pamoja na kuwabaka wanawake na wasichana.
Wakati huo huo, Umoja wa Afrika huenda ukachukua jukumu la kusimamia usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati huu juhudi za kikanda zikiendelea huku mikanganyiko ikishuhudiwa kuhusu maamuzi ambayo yamekuwa yakichukuliwa.
Kumepangwa kufanyika mkutano wa pande tatu utaoyakutanisha mashirika yote ya kikanda, SADC, EAC na ICGLR lengo ikiwa ni kupanga uratibu wa michakato iliopo na kukubaliana juu ya vikosi mbalimbali vya kikanda hususan vile vya ukanda wa Afrika mashariki vilivyo huko tangu Oktoba mwaka 2022. Serikali ya Kinshasa imekosoa utendaji kazi wa vikosi vya Afrika Mashariki ambavyo imesema havikabiliana na waasi ipasavyo na sasa inataka vikosi vikosi vya SADC viingie nchini humo vikiwa na uwezo kamili wa kushambulia waasi.
342/