20 Mei 2023 - 14:14
Kuendelea mgogoro huko Sudan kwa kuuzuliwa Hamidti katika Baraza la Uongozi wa Mpito

Mgogoro wa kisiasa na vita vingali vinaendelea huko Sudan licha ya kufanyika mazungumzo na jitihada za upatanishi nchini humo. Katika hatua ya karibuni, Jenerali Abdel Fattah al Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan ametoa amri ya kumuuzulu Mohamed Hamdan Dagalo (Hamidti) katika nafasi ya Naibu Mkuu wa baraza hilo.

Jenerali Abdel Fattah al Burhan jana Ijumaa alitoa dikrii ya kumuuzulu wadhifa huo Hamdan Dagalo na kisha kumteua Malik Agar mjumbe wa baraza hilo kuwa Naibu Mkuu wa Baraza la Uongozi wa Mpito la Sudan. Wakati huo huo al Burhan amewateua Luteni Jenerali Shamsuddin Kabashi Ibrahim kuwa Kaimu Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi, Luteni Jenerali Yasir Abdulrahman Hasan Al-Ata kuwa msaidizi wa Mkuu wa vikosi vya ulinzi na mhandisi Ibrahim Jabir kuwa msaidizi wa kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Sudan. 

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan tokea Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo chini ya uongozi wa Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya usaidizi wa haraka (RSF) vinavyoongozwa na Kamanda Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la (Hamidti); ambapo al Burhan na Hamidati hadi sasa wameshindwa kutatua hitilafu baina yao. Hitilafu hizo zilipamba moto kuhusiana na kujiunga jeshini vikosi vya usaidizi wa haraka (.RSF), na zilikuwa chanzo cha kuanza vita huko Sudan.  

Al Burhan ambaye anaongoza jeshi la Sudan amevituhumu vikosi vya usaidizi wa haraka na kutangaza kuwa kile kilichojiri wiki kadhaa zilizopita huko Sudan zilikuwa juhudi zilizofeli za waasi zenye malengo kamili ya kisiasa za kutaka kutwaa madaraka ya nchi. Al Burhan ameongeza kuwa kitendo hicho kilikuwa mradi wa kutaka kuipora nchi ya Sudan na historia yake yote kwa ajili ya mkakati wa kuunda serikali ya mamlaka ya mtu mmoja. Wakati huo huo, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Hamidti) anamtuhumu al Burhan kwa usaliti na kujaribu kuwapindua shakhsia wa serikali ya zamani ya Sudan wakiwemo wafuasi wa Omar Hassan al Bashir. 

Ala Kul haal, moto wa vita umepamba moto tena huko Sudan; na licha ya mapatano yaliyofikiwa huko Jeddah, lakini pande zinazozozana zinaendelea kuhujumiana kila uchao. Ripoti zinaarifu kuwa Khartoum mji mkuu wa Sudan umeshuhudia mashambulizi makali ya anga na mapigano ya umwagaji damu kati ya pande hasimu huku mashambulizi ya anga katika mji mkuu huo yakiendelea. 

Hali hii ya mambo imempelekea Martin Griffiths Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kibinadamu huko Sudan kulaani ukiukaji wa makubaliano ya Jeddah.

Pande hasimu huko Sudan zinafanya kila ziwezalo ili kutwaa madaraka ya nchi licha ya jitihada zote zilizofanywa hadi sasa za kusitisha mapigano kati ya pande hizo. Aidha chini ya kivuli cha kujaribu kusaka amani huko Sudan pande za kigeni zinaendelea kuchochea vita kwa maslahi yao. Bila shaka ni wazi kuwa uungaji mkono wa nchi za nje kwa pande zinazozozana huko Sudan umezipelekea pande hizo kujiamini kiuwezo juu ya kuibuka mshindi vitani na hivyo kupuuza mapatano waliyofikia hadi sasa. 

Hii ni katika hali ambayo wananchi wa Sudan ambao kwa muda sasa wamekuwa na matumaini ya kuona nchi yao ikirejea katika amani na uthabiti; wanaona ndoto zao zikiwa zimetoweka, bali wanakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi, kiafya na ukosefu mkubwa wa chakula. Kuhusiana na suala hilo Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa: Kunahitajika msaada wa kibinadamu wa karibu yuro bilioni 3 kwa ajili ya Sudan. 

Ramesh Rajasingham Mjumbe na Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa anasema kuhusu suala hilo kwamba: Wananchi wa Sudan wanashindwa kujidhaminia mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na huduma za afya. Karibu watu milioni moja wamekimbia mapigano huko Sudan na kukimbilia katika nchi jirani. Wakati huo huo karibu watu milioni 25 yaani zaidi ya nusu ya jamii ya nchi hiyo wanahitaji misaada ya kibinadamu na makazi.  

Licha ya kutolewa indhari na kufanyika juhudi mbalimbali, lakini pande hasimu huko Sudan zinaendelea kupigana, na inaonekana kuwa ukiachilia mbali madhara ya kisiasa, raia wa  nchi hiyo ndio waathirika wakuu wa mzozo unaoendelea huko Sudan. 

342/