Katika ujumbe aliotuma Umoja wa Mataifa, al Burhan amedai kuwa Volker Perthes, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, alimhamasisha Mohammad Hamdan Dagalo, kamanda wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) kuanzisha uasi nchini Sudan.
Al Burhan ameongeza kuwa: Kuwepo kwa Perthes kama mkuu wa ujumbe wa kidiplomasia wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan hakusaidii utekelezaji wa kazi za ujumbe huo za kuunga mkono kipindi cha utawala wa mpito.
Kamanda wa jeshi la Sudan pia amemstuhumu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kuwa amepotosha maoni ya umma katika ripoti yake.
Volker Perthes aliondoka katika mji wa Port Sudan na kuelekea New York Jumamosi iliyopita baada ya kupokea vitisho vya kufukuzwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo.
Mwezi Januari 2021, Perthes ambaye ni raia wa Ujerumani aliteuliwa kuwa mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mkuu wa ujumbe wa kidiplomasia wa umoja huo kusaidia Sudan wakati wa kipindi cha mpito.
Mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na askari wa Kikosi cha radiamali ya Haraka (RSF) yameitumbukiza nchi hiyo kwenye lindi la machafuko. Hifadhi ya chakula, fedha taslimu na vitu muhimu vinapungua kwa kasi, huku uporaji mkubwa ukiathiri benki, balozi, maghala ya bidhaa za misaada na mahospitali.
342/