31 Mei 2023 - 13:53
WFP: Mgao wa chakula kwa wakimbizi Tanzania kupunguzwa kwa 50%

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, litapunguza mpango wa mgawo wa chakula kwa wakimbizi walioko nchini Tanzania kuanzia mwezi ujao wa Juni.

Taarifa ya WFP imeeleza kuwa, zaidi ya wakimbizi 200, 000 nchini Tanzania watapewa tu nusu ya mgao wa chakula kuanzia mwezi ujao kutokana na ukosefu wa fedha za wafadhili.

Kupunguzwa kwa mgao wa chakula kwa mara ya pili nchini Tanzania katika miezi ya hivi karibuni, kunafuatia hatua kama hizo kote duniani huku shirika hilo la Umoja wa Mataifa likikabiliwa na ukata fedha taslimu na kupanda kwa bei ya chakula, hasa kutokana na vita vya Ukraine.

Sehemu nyingine ya taarifa ya WFP imeeleza kwamba, mgao wa chakula kwa wakimbizi nchini Tanzania ambao asilimia 70 kati ya wakimbizi hao ni kutoka Burundi na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umepunguzwa kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2020.

Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa mamia ya wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchini humo tangu mwaka 2015 baada ya mzozo wa kisiasa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo hayati Pierre Nkurunziza.

Maafisa wa serikali ya Tanzania na Burundi wamekuwa wakihimiza wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchini Tanzania kurudi nyumbani wakisema kwamba, amani imerejea na hakuna sababu za kuendelea kuishi ukimbizini nchini humo.

Huku nyuma pia Tanzania imerwahi kulaumiwa baada ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutangaza uamuzi wa kuwarejesha nyumbani kwa nguvu wakimbizi wa Burundi walioko nchini humo.

342/