Iran imeionya Korea Kusini kwamba ushiriki wowote wa kijeshi katika Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz utachukuliwa kuwa uungaji mkono wa moja kwa moja kwa upande unaofanya uchokozi dhidi ya Iran, na kwamba hatua hiyo inaweza kuwa na madhara makubwa.
Ofisi ya Rais wa Korea Kusini imekanusha taarifa zinazoeleza kuwa Seoul imeamua kutuma vikosi katika Mlango-Bahari wa Hormuz, na kutangaza kwamba maelezo kuhusu ushiriki wa nchi hiyo katika kuhakikisha utulivu wa kikanda bado hayajakamilishwa, huku mazungumzo ya kiusalama na Marekani katika suala hilo yakiwa hayajapiga hatua.
Jarida la The Atlantic limeandika kuwa Donald Trump, badala ya kukubali jukumu la kushindwa katika vita dhidi ya Iran, ameelekeza shinikizo kwa washirika wa Marekani. Jarida hilo linasema Korea Kusini imekuwa miongoni mwa walengwa wa hatua hizo, licha ya kuwepo kwa makumi ya vichwa vya nyuklia vya Korea Kaskazini.