15 Machi 2025 - 14:22
Imam Khamenei: Kitendo chochote kibaya cha kijeshi cha Marekani na Mawakala wake, kitapata jibu thabiti na la uhakika

Imam Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alikutana na maelfu ya Wanafunzi wa vyuo vikuu, wawakilishi kutoka Jumuiya za Wanafunzi wa Kisiasa, Kijamii na Kiutamaduni na makundi mbalimbali ya Jihadi. Mkutano huo ulifanyika katika Husseiniyyah ya Imamu Khomeini (MA), mnamo Machi 12, 2025.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AhlulBayt (a.s) - ABNA - : Imam Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alikutana na maelfu ya Wanafunzi wa vyuo vikuu, wawakilishi kutoka Jumuiya za Wanafunzi wa Kisiasa, Kijamii na Kiutamaduni na makundi mbalimbali ya Jihadi. Mkutano huo ulifanyika katika Husseiniyyah ya Imamu Khomeini (MA), mnamo Machi 12, 2025.

Mwanzoni mwa Mkutano huu, Kiongozi Muadhamu alisisitiza juu ya mapendekezo muhimu kuhusu kuimarishwa utambulisho wa Wanafunzi, kwa kutoa tajriba mbili tofauti za vijana wa Kiiran katika makabiliano yao na nchi za Magharibi. "Uzoefu wa kwanza ulisababisha hisia ya hasara ya kibinafsi (kujipoteza mwenyewe).

Hata hivyo, katika tajriba ya pili, ambayo inalingana na harakati za sasa za kundi la Wanafunzi, utambuzi wa hali halisi ya Magharibi, harakati za kutafuta uhuru, na kujiweka mbali na changamoto zinazoletwa na ustaarabu wa Magharibi limekuwa jambo kuu (muhimu)," alisema.

Katika matamshi yake kuhusiana na mazungumzo na Marekani, Imam Khamenei aliashiria nukta kadhaa, akirejelea kauli zilizotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu utayarifu wa Marekani kwa mazungumzo na makubaliano, na barua aliyoituma kwa Iran. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja vitendo hivyo kuwa ni kujaribu kuhadaa maoni ya umma wa kimataifa na kusema, "Bado sijapokea barua hii, lakini Marekani inataka kueneza uwongo kwamba 'Iran haitaki kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano, tofauti na sisi. Hata hivyo, mtu binafsi anayetoa madai haya ni mtu yule yule aliyerarua matokeo ya mazungumzo yetu ya awali na Marekani. Tunawezaje kujadiliana na mtu ambaye tunajua hataheshimu ahadi zao?">

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akirejea makala katika gazeti moja inayosema kuwa "kutokuwa na imani baina ya pande mbili katika hali ya vita kusizuie mazungumzo," alisema kwamba madai hayo si sahihi. Alieleza kuwa ikiwa pande zinazojadiliana hazina imani na uaminifu na dhamira ya upande wa pili kwa matokeo ya mazungumzo yao, hazitashiriki mazungumzo, kwani mijadala hiyo itakuwa ya bure na haina maana yoyote.

Aliendelea kusema kuwa, "Tangu mwanzo, lengo letu katika mazungumzo limekuwa ni kuondolewa kwa vikwazo, ambavyo kwa bahati nzuri vinapoteza athari zake taratibu kadri mchakato unavyoendelea." 

Imam Khamenei alisisitiza kwamba baadhi ya Wamarekani pia wanaamini kwamba kurefushwa kwa vikwazo kutapunguza athari zao. "Zaidi ya hayo, nchi iliyoidhinishwa itatafuta njia za kukwepa vikwazo hivi, na sisi pia tumegundua mbinu mbalimbali za kufanya hivyo," aliongeza.

Katika kujibu madai ya Marekani kwamba wataizuia Iran kupata silaha za nyuklia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema, “Kama tungetaka kutengeneza silaha za nyuklia, Marekani isingeweza kutuzuia.Hatumiliki silaha za nyuklia wala kuzifuatilia, kwani hatutaki silaha hizo kwa sababu ambazo tumeshazijadili".

Imam Khamenei amepuuzilia mbali vitisho vya Marekani vya kuchukua hatua za kijeshi na kusisitiza kuwa, "Tishio la kutoa pigo na kuanzisha vita sio mchakato wa upande mmoja. Iran ina uwezo wa kufanya mashambulizi na bila shaka itafanya hivyo."

Imam Khamenei ameongeza kuwa, "Iwapo Marekani na mawakala wao watachukua hatua mbaya, wao ndio watakaopata madhara makubwa zaidi. Bila shaka, vita si jambo zuri. Sisi hatutafuti vita. Hata hivyo, ikiwa mtu atachukua hatua [dhidi yetu], jibu letu litakuwa thabiti na la uhakika."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Marekani kuwa iko kwenye njia ya kuelekea kwenye udhaifu na kusisitiza kuwa, kwa upande wa uchumi wake, sera za kigeni, sera za ndani, masuala ya kijamii na nyanja nyinginezo mbalimbali, Marekani iko katika hali ya kuzorota na haiwezi tena kushikilia madaraka iliyokuwa nayo miaka 20 hadi 30 iliyopita.

Zaidi ya hayo, alisema kuwa mazungumzo na utawala wa sasa wa Marekani sio tu kwamba yanashindwa kuondoa vikwazo, bali pia yanasaidia kuficha utatuzi wa vikwazo hivyo, huku yakizidisha shinikizo na kuruhusu madai (matakwa) mapya ya kupita kiasi yaweze kujitokeza.

Kwingineko katika matamshi yake, Imam Khamenei alizitaja Harakati za Mapambano huko Palestina na Lebanon kuwa zenye nguvu na ari zaidi kuliko hapo awali. “Kinyume na matarajio ya adui, si Upinzani (Muqawamah)  wa Palestina wala ule wa Lebanon ulioyumba; badala yake, wamekuwa na nguvu zaidi na wenye (ari mpya na) msukumo zaidi. Ingawa (mauaji haya na) vifo hivi vya kishahidi vimewasababishia hasara ya Kibinadamu, lakini wakati huo huo vimeimarisha motisha yao, "alibainisha.

Katika hali hiyo hiyo, ameongeza kuwa, "Mtu kama Sayyid Hassan Nasrallah anaweza kuondoka kwenye kundi hili, na kuacha pengo; hata hivyo, katika siku za baada ya kuuawa Shahidi, hatua ambazo Hezbollah ilichukua dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni zilikuwa na nguvu zaidi kuliko juhudi zake za awali."

Kuhusu Muqawamah wa Palestina, Imam Khamenei alibainisha: "Katika Muqawamah wa Palestina, watu binafsi kama vile Shahidi Ismail Haniyeh, Shahidi Yahya Sin'war na Mohammed Deif hawako tena miongoni mwao. Hata hivyo, wakati huo huo, wanaweza kuweka masharti yao kwa upande unaopingana nao (kwa hasimu wao) katika mazungumzo, ambayo utawala wa Kizayuni, waungaji mkono wake, na Marekani wamesisitiza juu yake."

Imam Khamenei amesisitiza tena uungaji mkono usioyumba wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Muungano wa Mapambano ya Muqawamah na kudai kuwa: "Viongozi wa Iran, ikiwemo Serikali na Rais wameungana katika ahadi zao za kutoa uungaji mkono kamili kwa Mapambano ya Muqawamah wa Palestina na Lebanon. Mwenyezi Mungu akipenda Taifa la Iran litaendelea kusimama kidete kama kinara wa Muqawamah dhidi ya dhulma kama ilivyokuwa huko nyuma."

Kwingineko katika salamu zake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha matukio mbalimbali ya mwaka uliopita na kusema: "Mara hii mwaka jana, tulikuwa na Shahidi Raisi miongoni mwetu, Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Shahidi Ismail Haniyeh, Shahidi Sayyid Hashim Safiyyud-Din, Shahidi Yahya Sin'war, Shahidi Mohammad Deif, na wengine kadhaa mashuhuri. Hata hivyo, hawako nasi tena, na huku kutokuwepo kwao kumesababisha adui kuamini kwamba tumezidi kuwa dhaifu." Aliongeza zaidi: "Ninaweza kuthibitisha kwa ujasiri kwamba ingawa kukosekana kwa ndugu hawa wa thamani ni hasara kwetu, katika mambo mengi tumekuwa na nguvu zaidi ikilinganishwa na mwaka jana, na hatujadhoofika pia katika maeneo fulani."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameona kuibuka harakati za makabiliano zinazoongozwa na wanafunzi dhidi ya Marekani kuwa ni hatua muhimu ya kuleta mabadiliko makubwa, ambayo ilitolewa mfano na mwamko wa tarehe 7 Disemba 1953 wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran katika kukabiliana na ziara ya Nixon. Maandamano haya, ambayo yalisababisha kuuawa Shahidi kwa Wanafunzi watatu mikononi mwa utawala wa Pahlavi, yalionekana kuwa dhihirisho la wazi la asili ya kweli (halisi) ya Magharibi ambayo ilifichuliwa.

Katika hali hiyo hiyo, Imamu Khamenei alibainisha kuendelea kuwepo kwa chuki na nchi za Magharibi, hata katika kukabiliana na kudhoofika kwake kabla ya ushindi wa Mapinduzi. "Kama Mapinduzi hayangetokea mwaka wa 1979, nchi ingekuwa kwenye njia inayoongoza kwa kuongezeka kwa utegemezi wa kigeni, na kunyimwa marupurupu yake yote na utajiri wa kiroho," alisema.

Akirejelea juhudi zisizo na kikomo za wanyanyasaji wa kimataifa katika mapambano na njama zao dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: "Wanasema 'Tunatangulia sisi kwanza,' maana yake ni kwamba dunia nzima inapaswa kutanguliza masilahi yao kwanza kuliko ya kwao. Mtazamo huu wa kujitakia (kulitanguliza Taifa lako katika maslahi) ndio ambao kwa sasa unaozingatiwa na kila mtu ulimwenguni kote. Hivi leo, Iran ya Kiislamu ndiyo nchi pekee ambayo imesisitiza kwa uthabiti kwamba kamwe, kwa hali yoyote ile, haitatanguliza masilahi ya wengine juu ya maslahi yake mwenyewe."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja madhumuni ya juhudi za adui hususan kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano kuwa ni jaribio la kurejesha ushawishi na utawala wa Magharibi juu ya Iran na kufufua upya moyo wa kabla ya Mapinduzi, ambao ni moyo ya uzembe, utiifu, na utegemezi ndani ya wanafunzi na vijana wa Iran.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha