19 Machi 2025 - 18:25
Source: Parstoday
Katibu Mkuu wa UN asema ameshtushwa na mashambulio mapya ya Israel Ghaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, ameshtushwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya anga yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza yaliyoua shahidi mamia ya Wapalestina wakiwemo watoto na wanawake.

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN ameeleza katika taarifa kwamba, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza kwa msisitizo mkubwa kusitishwa mapigano mara moja, kuanzishwa tena uingizaji misaada ya kibinadamu huko Ghaza bila ya kizuizi na kuachiliwa mateka waliosalia.

Mamlaka za utawala katika Ukanda wa Ghaza zimetangaza kuwa mamia ya Wapalestina waliuawa shahidi na wengine wengi walitoweka wakiwa hawajulikani waliko ndani ya muda wa saa tano tu mara baada utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzisha tena vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo.

Utawala ghasibu wa Israel ulikubali kusitisha mapigano na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas kuanzia Januari 19, na pande hizo mbili zilikuwa katika mazungumzo ya kurefusha usitishaji mapigano kuelekea kwenye awamu ya pili ya makubaliano kabla ya Tel Aviv kuanzisha ghafla mashambulizi makubwa katikati ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, mbali na hatua iliyochukua zaidi ya wiki mbili nyuma ya kuzuia kikamilifu misaada yote ya kibinadamu kuingizwa katika Ukanda wa Ghaza.

Mashambulizi ya kinyama ya Israel yaliyoanza Oktoba 7, 2023 yameshaua shahidi zaidi ya Wapalestina 48,500 wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuigeuza Ghaza eneo la magofu.

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Ghaza.

Israel inakabiliwa pia na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwa vita vya kinyama ilivyoanzisha dhidi ya eneo hilo la Palestina.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha