Katika hali ambayo Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine amesisitiza siasa za kutoa mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Tehran, Iran inatilia mkazo kanuni za kuheshimiana pande mbili katika mazungumzo na kuchukulia mazungumzo yanayofanyika nje ya misingi hiyo kuwa jambo lisilokubalika kabisa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa ikipinga na kukabiliana na siasa za kijuba na vitisho za nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani. Inasisitiza kwamba haitaruhusu maslahi yake ya kitaifa na heshima ya watu wake kukanyagwa na nchi zinazojiona kuwa na nguvu na hivyo kujipa haki ya kukanyaga haki za wengine. Mivutano kati ya Iran na nchi za Magharibi imeongezeka katika siku za karibuni hivyo ni wazi kuwa kuelewa masharti ya Iran kwa ajili ya kufanya mazungumzo huenda kukasaidia katika kuelewa vizuri misimamo yake na hivyo kuimarisha uhusiano wake na nchi za Magharibi, jambo ambalo bila shaka litasaidia kuimarisha usalama wa kimataifa.
Mara tu baada ya Donald Trump kuingia tena katika Ikulu ya White House amerejesha siasa zake za kibabe za eti kutoa mashinikizo ya juu dhidi ya Iran, ambapo Iran nayo imetangaza rasmi kwamba kwa vyovyote vile haitakubali mazungumzo ambayo yatapuuza na kukanyaga heshima na mamlaka yake ya kitaifa. Msimamo huu umechukuliwa baada ya kauli za vitisho za Trump kuhusu uwezekano wa kutumia chaguo la kijeshi iwapo makubaliano hayatafikiwa na Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, mazungumzo yoyote yanapaswa kufanywa kwa misingi ya kuheshimiana pande mbili na kulinda heshima na maslahi ya kitaifa. Imesema wazi kwamba haitazungumza chini ya mashinikizo wala kuacha vitisho vipite bila kujibiwa.
Pia inasema makubaliano yanapasa kuwa ya kujenga na yenye dhamana ya kutekelezwa. Iran itakubali kufanya mazungumzo iwapo tu yatakuwa ni ya kujenga na yenye dhamana ya kutekelezwa, vinginevyo hayatakuwa na maana na yatakuwa ni kupoteza wakati tu.
Iran inataka kupunguza na kuondoa tofauti zilizopo kwa njia ya mazungumzo, lakini wakati huo huo haitakubali kutishwa kwa vitisho vya kushambuliwa kijeshi na mbinu nyingine zinazotumiwa na maadui.
Msimamo wa Iran dhidi ya mashinikizo ya kimataifa hususan siasa za Marekani unaashiria stratijia ya muda mrefu katika siasa zake za nje. Iran hataki jingine ghairi ya kulinda mamlaka yake ya kujitawala na heshima ya kitaifa, na inayachukulia mazungumzo yoyote ambayo yanatilia shaka suala hilo kuwa ni jambo lisilokubalika. Ni wazi kuwa msimamo wa nchi za Magharibi, hasa Marekani kuhusiana na hilo unaweza kuwa kikwazo kikubwa katika njia ya kufanikisha mazungumzo ya baadaye na Iran, na hivyo kuathiri vibaya mahusiano ya kimataifa.
342/
Your Comment