19 Machi 2025 - 18:27
Source: Parstoday
Iran yakosoa vikali uingiliaji wa nchi za Magharibi katika kazi za Baraza la Haki za Kibinadamu UN

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amezikosoa vikali baadhi ya nchi za Magharibi kwa kutumia vibaya taasisi za Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, nchi hizo zinataka kuingiza siasa katika masuala ya haki za binadamu dhidi ya Iran kwa kupuuza masuala ya kimsingi ya haki za binadamu ukiwemo mgogoro wa Palestina.

Akihutubia kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la UN jana Jumanne, Machi 18, 2025, Ali Bahreini alizikosoa vikali nchi ambazo zimeweka msingi wa kuchunguza hali ya haki za binadamu nchini Iran.

Amesema: “Mchezo huo wa kuchekesha unakera zaidi tunapogundua kuwa waigizaji wake wakuu ni Ujerumani na Uingereza; Nchi ambazo zenyewe zina historia mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu. Katika kipindi cha miezi 19 iliyopita, wakati jinai za Israel dhidi ya watu wa Palestina zilipofika kileleni, nchi hizi mbili sio tu hazijachukua hatua yoyote kukomesha jinai hizo, bali kwa himaya na misaada yao ya kifedha, kijeshi na kisiasa kwa utawala huu, zinahesabiwa kuwa washirika katika jinai zake na lazima ziwajibishwe mbele ya dhamiri za binadamu."

Iran yakosoa vikali uingiliaji wa nchi za Magharibi katika kazi za Baraza la Haki za Kibinadamu UN

Akiashiria nafasi ya nchi hizo katika kuwasilisha maazimio dhidi ya Iran, Bahreini amesisitiza kuwa: “Waasisi wa maazimio hayo wao wenyewe ndio wavunjaji wakuu wa haki za binadamu za watu wa Iran; Wamewazuia Wairani kupata haki zao za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa kuwawekea vikwazo vya upande mmoja na kinyume cha sheria, au kwa kutekeleza sera za mashinikizo ya juu kabisa, wamehatarisha haki ya maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho cha Iran."

Ameendelea kusema: "Nchi hizo hizo, katika mienendo yao ya kinafiki na kwa kupendekeza azimio dhidi ya Iran, zimefichua ukosefu wao wa uaminifu na hadhi katika kile kinachoitwa kutetea haki za binadamu. Nchi hizi (za Magharibi) hazina uhalali wa kushiriki katika mjadala wa haki za binadamu kuhusu nchi nyingine. Zinapanda tu mbegu za kukata tamaa katika Baraza la Haki za Kibinadamu la UN."

Balozi wa Iran katika Ofisi ya UN mjini Geneva amemalizia kwa kukumbusha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa mtetezi madhubuti wa ulimwenguu wa pande kadhaa, imedhihirisha wazi dhamira yake ya kukuza na kulinda haki za binadamu. "Tunaheshimu haki za binadamu kwa mujibu wa yale tuliyofunzwa na dini, historia na utamaduni wetu. Serikali na watu wa Iran wameonyesha kwamba hawataacha imani, uhuru na juhudi zao kwa ajili ya kudumisha amani na haki duniani", amesisitiza Bahreini. 

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha