8 Aprili 2025 - 20:05
Source: Parstoday
Ushuru wa Trump; Masoko ya hisa ya US yazidi kuporomoka

Hisa za Marekani zimeendelea kuporomoka kwa siku ya tatu mfululizo, huku mashirika na wawekezaji wakishindwa kuelewa malengo ya mipango mipya ya ushuru ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump.

Kiwango cha hisa za shirika la S&P 500 na hisa za wastani za kiwanda cha Dow Jones jana Jumatatu kilishuka kwa asilimia 0.23 na asilimia 0.91 mtawaliwa, na kupata hasara kwa siku ya tatu mfululizo.

Licha ya mtikisiko wa masoko ya hisa na matamshi ya wasiwasi ya viongozi wakuu wa biashara na wawezekezaji,  lakini Trump jana Jumatatu alidokeza kwamba anaweza kushadidisha vita vyake hivyo vya kibiashara.

Hiyo jana, jarida la Marekani la Newsweek liliripoti kupamba moto maandamano katika kona zote za Marekani kupinga siasa hizo za Trump na kusema: Maandamano ya taifa zima yaliyobebwa na kaulimbiu ya "Hands Off" (yaani acha uingiliaji) dhidi ya utawala wa Trump yamefanyika si tu katika majimbo yote 50 ya Marekani, Washington, D.C na Puerto Rico, bali pia katika nchi nyingi nje ya Marekani.

Trump amechochea mvutano na vita vya kibiashara kwa kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na ushuru wa 10% kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje na ushuru mkubwa zaidi kwa nchi kama vile China (34%), Umoja wa Ulaya (20%) na Japan (24%). 

Hatua hizi, mbali na kusababisha tetemeko kubwa katika masoko ya fedha duniani na kudhoofisha thamani ya sarafu ya dola ya Marekani, lakini zimezidisha wasiwasi kuhusu mdororo wa uchumi duniani.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha