Akizungumza Ijumaa jijini Tehran amesema: “Serikali [ya Iran] haijawahi kutegemea mazungumzo au maelewano [na Marekani] katika hatua zake, lakini wakati huohuo tunaamini kuwa tukifanikiwa kupata amani na utulivu, mafanikio yatakuwa mengi."
Kauli hiyo ameitoa wakati ambapo Iran na Marekani zinatarajiwa kufanya duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jijini Roma, Italia, leo Jumamosi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, na Steve Witkoff, mjumbe maalum wa rais wa Marekani kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi), waliongoza duru ya kwanza ya mazungumzo hayo mjini Muscat, mji mkuu wa Oman, tarehe 12 Aprili. Pande zote mbili zilieleza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa chanya.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Pezeshkian amesema kuwa Iran inatekeleza diplomasia ya kiutendaji katika kutatua matatizo ya kikanda na kimataifa.
Amesisitiza kuwa: “Hatutaki kuanzisha vita, bali tunajitahidi kutatua tofauti za kikanda na kimataifa."
Amebainisha kuwa Iran ni mhanga wa ugaidi na kwamba Wairani wapatao 25,000 wakiwemo wasomi na wanasayansi wameuawa katika hujuma za kigaidi.
Amesema kuwa utawala wa Israeli ndio chanzo kikuu cha ugaidi duniani, kwani unatekeleza vitendo vya kigaidi bila hofu popote duniani.
Rais wa Iran amekemea vikali baadhi ya nchi kwa kuiunga mkono Israel huku zikijidai kutetea haki za binadamu, akisema matendo ya utawala huo ni mauaji ya kimbari.
Amesema, “Haiingii akilini kuwa utawala fulani unaruhusiwa kutekeleza mauaji ya kulenga watu kila wakati upendavyo, huku wale wanaojiita watetezi wa haki za binadamu wakibakia kimya au hata kunga mkono utawala huo.”
Rais wa Iran amesisitiza kuwa ikiwa nchi za Kiislamu zingejionyesha kuwa na mshikamano na nguvu, Wazayuni na wengine wasingethubutu kufanya jinai dhidi ya Waislamu.
342/
Your Comment