Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) - ABNA - Sambamba na maadhimisho ya Siku Kumi za Karama - Dahe Karamat - (The Ten Days of Karama), Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa "Waandishi wa Habari wa Ahlul-Bayt (a.s)" umefanyika leo Alhamisi asubuhi, tarehe 1 Mei, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) katika Mji wa Qom, kwa ushiriki wa wanaharakati wa Habari na Wasomi kutoka Iran na Bara la Afrika.
Mkutano huu, ulioandaliwa kwa juhudi za Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) — ABNA — ulihudhuriwa na Ayatollah Reza Ramazani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s); Dkt. Sayyid Mohammad Amin Aghamiri, Katibu wa Baraza Kuu la Mtandao na Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Mtandao wa Taifa; Mohammadreza Sowgandi, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Idara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Mkoa wa Qom; pamoja na baadhi ya manaibu (wasaidizi) na wakurugenzi wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), Kituo cha Kitaifa cha Mtandao, na Taasisi nyingine husika. Vilevile, walihudhuria pia walimu kutoka Bara la Afrika kama wageni maalum.
Mwanzoni mwa hafla hii, wahariri wa tovuti za Kiswahili na Kihausa za Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) — ABNA — waliwasalimu na kuwakaribisha wageni kwa maneno mafupi kwa lugha zao za asili na kuutambulisha mkutano huu wa Waandishi wa Habari wa Ahlul-Bayt (a.s) kwa washiriki na Wanaharakati wa Habari kutoka Bara la Afrika kama mwanzo mpya wa mahusiano, ushirikiano na nguvu ya pamoja.
Baadaye, ujumbe wa video kutoka kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, pia ulionyeshwa katika hafla hii.
Mkutano huu ni hatua ya kwanza ya kutambua uwezo wa Wanahabari wa Kiislamu
Ayatollah Reza Ramazani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya AhlulBayt (a.s.) na mzungumzaji maalum wa hafla hii, akielezea shukrani kwa ubunifu wa Shirika la Habari la ABNA katika kuandaa mkutano huu na kusisitiza juu ya umuhimu na ulazima wa kuandaliwa kwa mkusanyiko huu, alisema: "Waandishi wa habari wa AhlulBayt (a.s.) wana uwezo wa kipekee, na hatua ya kwanza ni kuelewana na kutambua uwezo huu."
Aliendelea kusema kuwa uwezo huu umetokana na muujiza wa Qur'ani Tukufu, yaani Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambayo yaliibua mabadiliko ya kimataifa. Mapinduzi ya Kiislamu yamepelekea Uislamu kujitokeza kama nguzo kuu dhidi ya mfumo wa kiulimwengu wa utawala wa mabavu.
Sifa muhimu zaidi ya mapinduzi haya ni mwelekeo wake wa fikra za AhlulBayt. Tunaamini kuwa mwelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mwanga kutoka kwenye mwelekeo wa fikra za AhlulBayt (a.s.). Ikiwa mwelekeo huu utaeleweka kwa usahihi na kufahamika vizuri na jamii ya leo na dunia kwa ujumla, tutazidi kushuhudia mapokezi ya kila siku ya mwelekeo huu. Bila shaka, inapaswa kufanyika ufafanuzi wa kina na sahihi wa fikra hizi."
Ayatollah Ramezani aligusia masuala ya mitandao ya kijamii na athari zake, na kusema:
"Wakati mwingine mazingira haya ya kidijitali yanaweza kuwasilisha uhalisia kwa njia isiyo sahihi, na kuyadhihirisha mambo ya uongo kana kwamba ni ya kweli. Kwa mfano, tukio la Arbaeen ni tukio kubwa sana, lakini halipewi uwasilishaji unaostahili. Hata hivyo, iwapo huko Ulaya watu wachache watatukana imani zetu, dunia nzima itajua haraka kuhusu hilo."
"Wajibu wa vyombo vya habari, kwa maana halisi ya neno, ni kuwasilisha ukweli. Hatupaswi kuangalia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa mtazamo wa Ki_Machiaveli. Magharibi hutumia mitandao ya kijamii ili kupanua mamlaka yao, lakini mtazamo wetu unapaswa kuwa wa kibinadamu na wa ukweli."
Jihadi katika uwanja wa vyombo vya habari sio jihadi ndogo kuliko jihadi ya kimwili
Ayatollah Ramazani aliendelea kwa kusema:
"Leo hii, jihadi katika uwanja wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii haiko chini ya thamani ya jihadi katika uwanja halisi wa vita (jihadi ya kimwili). Wote waliopo hapa wanashiriki katika kazi hii kwa roho ya kujitolea (jihadi), na tunatumaini kuona matokeo mazuri kupitia uandishi wa habari katika nchi zao."
"Sisi tuna utajiri mkubwa wa maudhui, na utajiri huu wa maudhui lazima uwasilishwe vyema katika anga ya mitandao ya kijamii."
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya AhlulBayt (a.s.) alihitimisha kwa kusema:
"Katika uwanja wa akili bandia (Artificial Intelligence), tunapaswa kufikia kiwango cha uzalishaji wa maudhui kinachokidhi mahitaji yetu. Hakuna aina ya maudhui ulimwenguni yenye thamani kama ile ya AhlulBayt (a.s.). Iwapo tutawasilisha maudhui haya kwa njia zenye mvuto na zenye athari katika mitandao ya kijamii, tunaweza kufanikia ushindi katika nyanja hii."
"Kwa kuzingatia sifa za ustaarabu wa Kiislamu, tuna uwezo wa kuwa washindi katika uwanja wa fikra duniani. Ili kufanikisha hilo, taasisi kama Kituo cha Kitaifa cha Mtandao zinapaswa kuchukua hatua zaidi katika kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuwasilisha maudhui ya Kiislamu na kidini kwa njia zenye mvuto na staha."
"Tunahitaji kuitambulisha Dini ya Kiislamu kwa njia sahihi na kamilifu — si kwa njia ya upotoshaji kama inavyoenezwa Magharibi. Uislamu wa AhlulBayt unatofautiana sana na aina za Uislamu zinazowasilishwa na baadhi huko Magharibi. Wakati huko wanajaribu kufuta au kuunganisha Uislamu na utamaduni wa Magharibi, sisi tunapaswa kuutambulisha Uislamu kwa ukamilifu wake na asili yake halisi."
Msisitizo wa Sheikh Ibrahim Zakzaky kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kueneza mafundisho ya AhlulBayt (a.s.)
Sheikh Ibrahim Zakzaky, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, katika ujumbe wake kwa mkutano huu alisisitiza umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kueneza mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s) na kusema:
"Tunapaswa kutumia uwezo wa vyombo vya habari ili kufikisha ujumbe wa AhlulBayt (a.s.) kwa watu. Hii ni wajibu unaowakabili vyombo vya habari kama Shirika la Habari la ABNA, ambalo limeunda mazingira mazuri kwa ajili ya kusambaza mafundisho haya."
Alitoa shukrani kwa hekima ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu (Ayatollah Khamenei) kwa kuanzisha Jumuiya ya Kimataifa ya AhlulBayt (a.s), pamoja na juhudi za Ayatollah Ramazani katika kuwezesha kufanyika kwa mkutano huu.
Alionyesha matumaini kuwa mikutano kama hii itaendelea kuandaliwa zaidi katika siku zijazo, na kwamba harakati za vyombo vya habari vinavyohusiana na AhlulBayt (a.s) zitaendelea kuenea kwa nguvu na uthabiti.
Teknolojia za kisasa ni fursa ya kueneza mafundisho ya AhlulBayt (a.s.)
Dkt. Sayyid Mohammad Amin Aghamiri, mjumbe wa Baraza Kuu la Mtandao na Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Mtandao wa Taifa, katika hotuba yake alieleza:
"Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeshuhudia mageuzi makubwa katika nyanja za vyombo vya habari na usimamizi wa masuala ya kiutamaduni. Hapo awali, lugha ilikuwa kizuizi kikubwa cha kusambaza maudhui, lakini leo kwa kutumia teknolojia za kisasa, maudhui hutafsiriwa na kusambazwa kwa lugha mbalimbali ndani ya sekunde chache."
"Mabadiliko haya ni fursa muhimu ya kueneza mafundisho ya AhlulBayt (a.s.) kwa ulimwengu mzima, lakini pia ni tishio kwa sababu kuna maudhui yanayokinzana na maadili yetu yanayoenezwa kwa kasi hiyo hiyo."
Aghamiri aliongeza kwa kusisitiza nafasi ya mitandao ya kijamii na vyombo vidogo vya habari (micro-media):
"Leo, athari ya vyombo vya habari vidogo ni kubwa zaidi kuliko ile ya vyombo rasmi vya habari. Tunapaswa kutumia uwezo huu kuzalisha maudhui kwa wingi, yenye mvuto na ubora."
"Akili bandia (AI) pia ni zana yenye nguvu inayopunguza gharama na kuongeza kasi ya uzalishaji wa maudhui, hivyo kusaidia kusambaza ujumbe wa kimaadili."
Alisisitiza kuwa:
"Upatikanaji wa haraka na wenye maarifa ya teknolojia hizi unaweza kutupa faida ya kiushindani katika uwanja wa vyombo vya habari. Tukisubiri, nafasi hiyo itapatikana kwa wote na tutapoteza fursa yetu ya kipekee."
Kuanzia msisitizo juu ya jihadi ya Vyombo vya Habari hadi kuwasilisha changamoto za Wanaharakati
Katika kuendelea kwa hafla hii, wanahabari watatu waliwakilisha kundi la wanaharakati kutoka Afrika na kueleza changamoto na mitazamo yao.
Salati Bello, mwanahabari kutoka Nigeria, alieleza umuhimu wa vyombo vya habari katika dunia ya leo na kusema:
"Inatosha kusema kuwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kwamba kama hakuwa kiongozi, angechagua kuwa mwanahabari. Hii inaonyesha nafasi ya juu ya vyombo vya habari katika jamii."
Salati Bello alitaja mkutano huu kuwa ni fursa nzuri ya ushirikiano na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanahabari, na akaongeza:
"Tunamuomba Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) kuongeza msaada na ushirikiano wa pande mbili na Muungano wa Wanafunzi na Wasomi wa Afrika."
Bi.Balqis Salihu kutoka Nigeria pia alizungumza katika mkutano huo, akieleza umuhimu wa vyombo vya habari katika maisha ya kila siku, na kutoa wito kwa wafuasi wa Madhehebu ya AhlulBayt (a.s.) barani Afrika — hasa Wanawake — kushiriki zaidi katika shughuli za Vyombo vya Habari.
-----
Bi.Balqis Salihu, akirejea maneno ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari, alitoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa ya AhlulBayt (a.s.) kuandaa warsha na kozi za mafunzo katika sekta ya habari na mawasiliano, ili wanawake pia waweze kushiriki kikamilifu katika kusambaza mafundisho ya AhlulBayt (a.s.) katika enzi hii ya kisasa.
Ibrahim Abu Aqil, Mwanahabari kutoka Nigeria, katika hotuba yake alielezea umuhimu mkubwa wa kazi ya vyombo vya habari katika kueneza mafundisho sahihi ya Ahlul-Bayt (a.s) na Uislamu wa kweli. Alisema:
“Ili kufanikisha lengo la kuwafikishia watu ukweli, tunahitaji mpango madhubuti na wa kina.”
Akaendelea kubainisha changamoto kadhaa zinazokwamisha juhudi hizi, zikiwemo:
- Ukosefu wa uelewa sahihi kuhusu usimamizi wa vyombo vya habari.
- Upungufu wa elimu ya dini inayohitajika kwa wanahabari.
- Kutokuwepo kwa taasisi rasmi za kuwafundisha na kuwaunga mkono wanahabari wa Kiislamu.
Abu Aqil pia alizungumzia changamoto za kiuchumi zinazowazuia vijana kutekeleza kikamilifu shughuli zao kwenye mitandao ya kijamii. Alisema:
"Kuna vijana wengi wenye elimu na akili, ambao wanaweza kufanya kazi nzuri katika mitandao ya kijamii, lakini kutokana na matatizo ya kiuchumi, hawawezi kutimiza majukumu yao katika uwanja huu."
Akaendelea kueleza kuwa suluhisho la matatizo haya ni kufufua na kuandaa upya warsha za mafunzo kwa ajili ya vijana barani Afrika, na kuongeza:
"Kwa kuwafundisha vijana jinsi ya kusimamia kitaalamu kazi za mtandaoni na kuwapa msaada wa kimkakati wanafunzi wa Kiislamu wa Kiafrika ili washiriki katika kazi za vyombo vya habari, matatizo haya yanaweza kutatuliwa."
Harufu nzuri ya uturi ya Haramu ya Imamu Mkarimu na Bibi wa Ukarimu Yaziburudisha Nyoyo za Washiriki ndani ya Ukumbi wa Mkutano
Katika sehemu maalum za hafla hiyo, baada ya usomaji mzuri wa Qur'an Tukufu kutoka kwa Sheikh Rajab Shaaban kutoka nchini Tanzania, na Qaswida nzuri ya pamoja na ya kupendeza kutoka kwa kikundi cha Qaswida cha Kimataifa cha Ahbab Bilal / Wapenzi wa Bilal (kinachoundwa na vijana kutoka Comoro, Uganda, Tanzania na Ivory Coast), kuwasili watumishi wa Haramu ya Bibi Maasumah (s.a) kuliijaza hafla hiyo hisia ya pekee, huku wageni wakibarikiwa na harufu nzuri ya uturi na Baraka za Bendera ya Kuba ya Haramu ya Bibi wa Ukarimu.
Usomaji wa mashairi kutoka kwa Bi.Asma Makhloufi kutoka nchini Algeria, kwa mnasaba maadhimisho ya Siku Kumi za Karama, pamoja na droo ya kutoa msaada wa kifedha kwa safari ya ziara ya Mashhad pia vilileta furaha isiyoelezeka, na hamu ya kutembelea Haramu ya Imam Ali bin Musa al-Ridha (a.s) ikajaza nyoyo za washiriki kwa shauku kubwa, furaha na upendo.
Aidha, kutajwa kwa jina la "Sayyid wa Muqawama" (Kiongozi wa Mapambano ya Kiislamu) kupitia Rouhollah Soleimani, Mratibu na Mwendesha Programu hodari wa hafla hiyo, pamoja na kuonyeshwa kwa video fupi ya kumbukumbu ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, kuliamsha kumbukumbu ya shujaa huyu na Mashahidi wengine wa Muqawama waliotangulia mbele ya haki.
Uzinduzi wa Mchakato wa Usajili wa Muungano wa Kimataifa wa Wanahabari Wanaohusiana na Ahlul-Bayt (a.s)
Katika sehemu nyingine ya hafla hiyo, Hassan Sadraei Aref, Mhariri Mkuu wa Shirika la Habari la ABNA, alikaribisha wageni na kusema kuwa mkutano huu wa kimataifa ni fursa ya kuzindua tovuti mpya ya shirika hilo, ambayo sasa inaungwa mkono kwa lugha 27 tofauti. Alisisitiza kuwa:
"Shirika la habari la ABNA ni nyumba ya wanahabari wote waliodhamiria kutangaza mafundisho ya AhlulBayt(a.s.)."
Aliongeza kuwa:
"Moyo wa mshikamano na kushirikiana katika kusambaza mafundisho ya AhlulBayt(a.s.) ni jambo la lazima. Katika muktadha huu, usajili wa Muungano wa Kimataifa wa Wanahabari Wanaohusiana na AhlulBayt(a.s.), ambao habari zake zilitangazwa katika mkutano wa pili, sasa umeanza rasmi. Muungano huu utaanza kazi zake rasmi baada ya kufikia wanachama 1000."
Uzinduzi wa Tovuti Mpya ya Shirika la Habari la ABNA lenye Lugha 27 na Droo ya Safari ya Ziara Mash-Had, na Mkutano Kuhitimishwa
Kutoa Kadi ya Uandishi wa Habari ya Heshima kwa Rais wa Umoja wa Wanafunzi wa Afrika katika Mji wa Qom ilikuwa sehemu nyingine muhimu ya hafla hiyo. Ayatollah Ramezani alikabidhi Kadi hiyo ya Heshima kwa Hojjat al-Islam Muhammad Amin Sajo, Rais wa Umoja wa Wanafunzi wa Afrika.
Katika sehemu za mwisho za hafla hiyo, tovuti mpya ya Shirika la Habari la ABNA yenye lugha 27 ilizinduliwa rasmi. Katika uzinduzi huu, walihudhuria wafuatao:
-
Ayatollah Ramezani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt(a.s).
-
Dr. Mohammad Amin Aghamiri, Katibu wa Baraza Kuu la Teknolojia ya Habari na Rais wa Kituo cha Taifa cha Teknolojia ya Habari.
-
Mohammad Reza Sooghandeh, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utamaduni na Habari ya Mkoa wa Qom.
-
Hojjat al-Islam Meitham Gholaami, Kiongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Teknolojia ya Habari na Mjumbe wa Baraza la Siasa la ABNA.
-
Sheikh Jaafar Traoré na Sheikh Thani Abdulrahim, Wahadhiri na Wanazuoni kutoka Bara la Afrika.
Your Comment