19 Aprili 2025 - 20:40
Source: Parstoday
Araqchi: Uhusiano wa Iran na Russia ni imara na wa kimkakati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi ameutaja uhusiano wa Iran na Russia kuwa ni imara mno na kwamba Moscow ni mshirika mkuu na wa kistratijia wa Iran.

Sayyid Abbas Araqchi ameyasema hayo katika kikao chake na mwenzake wa Russia, Sergey Lavrov mjini Moscow ambako amekwenda kukabidhi barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kwa Rais wa Russia, Vladimir Putin. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemshukuru mwenzake wa Russia kwa ukarimu wake na kusema: "Jana nilikuwa na kikao mwafaka na kirefu na Bw. Putin na nilimkabidhi ujumbe wa maandishi kutoka kwa Kiongozi Muadhamu. Huo ni ujumbe kwa Bwana Putin na ujumbe kwa dunia nzima kwamba Iran inaitambua Russia kuwa mshirika wake mkuu na wa kimkakati na inashauriana nayo katika masuala muhimu." 

Abbas Araqchi ameongeza kuwa: "Uhusiano wa Iran na Russia haujawahi kuwa wa karibu na wenye nguvu katika historia kama ilivyo hivi sasa. Hivi majuzi tulitia saini mkataba wa pande zote na wa kistratijia mjini Moscow ambao unapanua uhusiano wetu hadi viwango vya juu zaidi."

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesisitiza kuwa Moscow inaunga mkono suluhisho la kidiplomasia la faili ya nyuklia ya Iran.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha