Meja Jenerali Hossein Salami ameyasema hayo katika kikao kilichofanyika kusini mwa mji wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa nchi, akizungumzia vitisho vya Marekani kwamba Washington inaweza kuishambulia Iran iwapo mazungumzo yanayoendelea ya kuchukua nafasi ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 hayatazaa matunda.
"Tunamjua adui kikamilifu na tunafuatilia mienendo yake. Hata sasa, wakati mawasiliano ya kisiasa na mazungumzo yanapoendelea, tunasimama kwa izza na uthabiti, na yeyote atakayethubutu kukabiliana na Iran ya Kiislamu atasambaratishwa," amesema.
Jenerali Salami ameeleza bayana kuwa, nguvu ya Iran "imestawi mara nyingi zaidi tangu mwaka jana" na kwamba maadui zake pia wanalifahamu hilo.
Amebainisha kuwa Iran haitegemei kambi ya Muqawama kwa ajili ya ulinzi, lakini iwapo itakabiliwa na vitisho, mrengo wa Muqawama utachukua hatua madhubuti kulihami taifa hili.
Jenerali Salami amekanusha madai kwamba kambi ya Muqawama imedhoofishwa na mashambulizi ya Israel katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, akisisitiza kwamba, operesheni za hivi karibuni zinathibitisha kinyume chake.
"Maadui waliamini kwamba mrengo wa Muqawama ulikuwa umedhoofika, lakini wameona kwamba Gaza imeimarika zaidi. Yemen sasa inashambulia kwa ufanisi zaidi kwa makombora, na Hizbllah imerejesha nguvu zake," ameongeza Jenerali Salami na kubainisha kwamba, utawala wa Kizayuni "umepatwa na mfadhaiko na hamaki kutokana na hilo.
342/
Your Comment