Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AhlulBayt (a.s) -ABNA- Ayatollah al-Udhma Abdullah Jawadi Amuli, ambaye yuko ziarani nchini Iraq kwa ajili ya kutembelea maeneo matakatifu ya Kiislamu, amekutana na Ayatollah al-Udhma Sayyid Ali Sistani katika mji mtakatifu wa Najafu Ashraf.
Mkutano huu umefanyika katika mazingira ya kiroho na yaliyojaa ikhlasi, ambapo Marjaa hawa wawili wa kidini walibadilishana mawazo juu ya masuala muhimu ya kidini, kitamaduni na kijamii yanayohusu ulimwengu wa Kiislamu.
Katika fursa hiyo, Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli alimpongeza Ayatullah al-Udhma Sistani kwa nafasi yake ya juu ya kielimu na kiroho, na akatambua mchango wake mkubwa katika kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu na kutoa mwongozo kwa jamii za Kishia.
Ayatollah al-Udhma Sistani alieleza furaha yake kutokana na mkutano huu na akapongeza juhudi za kielimu na tafsiri za Ayatollah al-Udhma Jawadi Amuli.
Katika mkutano huo, Ayatollah al-Udhma Jawadi Amuli alimkabidhi Ayatollah Sistani zawadi ya tafsiri yake maarufu ya Qur’ani, “Tasnīm”, ambayo inahusisha juzuu 80 zilizochukua miaka 40 kuandikwa.
Ayatollah Sistani alipokea kazi hiyo ya kielimu kwa heshima maalum, akiisifu kwa maneno ya pongezi na kuitaja kama fahari kwa ulimwengu wa Kishia.
Alisisitiza umuhimu wa kulenga Qur’ani Tukufu katika elimu za kidini na akasema: Hadithi za Ahlul Bayt (a.s) zinapaswa kupimwa kwa mwanga wa Qur’an, kwani ni zile tu zinazolingana na Qur’ani ndizo zinazopaswa kukubaliwa na kutumika.
Ayatollah Sistani pia alisisitiza umoja kati ya vyuo vya kidini vya Kishia (hawza) akisema: “Maoni yetu kuhusu Hawza ya Qom hayapingani na yale kuhusu Hawza ya Najaf. Kwa uwezo wetu, tutazihudumia zote kwa moyo mmoja.”
Aidha, alisema: “Ninafahamu juhudi zako na hadhi yako ya kielimu. Tumesikia sana kuhusu sifa zako, lakini kuona kuna nguvu zaidi kuliko kusikia.”
Kwa upande wake, Ayatollah Jawadi Amuli alimpongeza Ayatollah Sistani kwa nafasi yake ya kipekee kama kiongozi mwenye huruma kwa wafuasi wa Ahlul Bayt (a.s) na watu wa Iraq, na akasema kuwa uwepo wake ni neema kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Pia alitambua nafasi ya kihistoria ya Marjaiyya (uongozi wa juu wa kidini) katika kulinda jamii ya Iraq na kupambana na mitazamo ya itikadi kali ya kikafiri (takfiri), akiutaja mchango wa Hawza ya Najaf kama chanzo kikuu cha baraka kwa Umma wa Kiislamu, moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Vyombo mbalimbali vya habari na taasisi za kidini vimekaribisha kwa furaha mkutano huu, wakiutaja kama hatua muhimu kuelekea mshikamano wa kielimu na umoja kati ya viongozi wakuu wa kidini wa Kishia.
Your Comment