30 Juni 2025 - 13:40
Source: Parstoday
Je, Iran imekabiliana vipi na bwabwaja za Trump dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi?

Bwabwaja na hambarara za Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu Imam Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran zimekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa viongozi wa Iran.

Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusiana na suala hili kwamba, kama kweli Trump anataka kufikia makubaliano na Iran, ni lazima aache kutoa matamshi ya dharau na yasiyokubalika dhidi ya Kiongozi Muadhamu, matamshi ambayo pia yanaumiza hisia na nyoyo za mamilioni ya wafuasi wake wa kweli.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: "Watu wakubwa na wenye nguvu wa Iran walioidhihirishia dunia kwamba utawala wa Israel hauna budi ila kumkimbilia "baba yake" Marekani, ili kuepuka kusambaratishwa na makombora yetu, hawatavumilia vitisho na matusi yanayotolewa na utawala huo dhidi ya viongozi wao. Iwapo hali hiyo itapelekea kufanyika makosa makubwa zaidi, Iran haitasita kufichua uwezo wake halisi, na hili bila shaka litaondoa uvumi wowote kuhusu uwezo wa Iran." Ameongeza kwa kusema: "Nia nzuri huleta nia nzuri, na heshima huleta heshima."

Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York pia umejibu vitishio vya kuuawa kigaidi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Marekani na utawala wa Kizayuni katika akaunti yake rasmi ya X kwa kusema: "Marekani na utawala wa Kizayuni zimetishia waziwazi kumuua Kiongozi Muadhamu. Kitendo hiki cha jinai ni mfano wa wazi wa ugaidi wa serikali ambao haupaswi kufumbiwa macho."

Kufuatia matamshi na vitisho visivyo na haya vinavyotolewa na watawala wa Marekani na Israel dhidi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mirsaeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amewaandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mwenyekiti wa Baraza la Usalama na Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akiwataka walaani vitisho hivyo kwa nguvu zao zote na kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya wanaotoa vitisho hivyo.

Katika barua hiyo mwakilishi wa Iran amesisitiza kuwa: Vitisho vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mfano wa wazi wa ugaidi wa serikali. Iravani ameongeza: "Tunatoa wito kwa Baraza la Usalama kutekeleza majukumu yake ya kisheria kuhusu matamshi haya ya jinai na uchochezi."

Je, Iran imekabiliana vipi na bwabwaja za Trump dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi?

Inaonekana kwamba bwabwaja za Trump kuhusu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu zinatokana na misimamo yake madhubuti dhidi ya misimamo ya kibeberu na ubabe wa Marekani dhidi ya mataifa mengine, ikiwa ni pamoja na msimamo wa Washington dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran. Imam Khamenei mara zote amekuwa akijibu kwa nguvu na bila uoga wowote vitisho vya kipumbavu vya Trump huku akiashiria misimamo ya kimantiki ya Iran na kusisitiza muqawama wa taifa la Iran dhidi ya uvamizi wowote wa adui dhidi ya Iran. Kufuatia ujumbe wa tatu wa televisheni wa Ayatullah Khamenei, baada ya utawala wa Kizayuni kuivamia Iran, kituo cha televisheni cha Marekani CNN kilitangaza kuwa: 'Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kutangazwa usitishaji vita kati ya Iran na Israel, Kiongozi Muadhamu wa Iran alituma ujumbe wa wazi kwa Rais Donald Trump wa Marekani kwamba Tehran kamwe haitasalimu amri.'

Rais wa Marekani ambaye anatumia kauli zinazokinzana na tabia zisizo na busara kuhadaa maoni ya umma, amekasirishwa mno na maneno ya Kiongozi wa Mapinduzi kuhusu kushindwa Marekani na hajaweza kuvumilia maneno hayo ambayo yameharibu kabisa simulizi na taswira zake zote za uwongo.

Nukta nyingine ni kwamba madai mapya ya Donald Trump kuhusu vikwazo dhidi ya Iran ni aina fulani ya jaribio la kuficha kushindwa kwa siasa zake za mashinikizo ya juu zaidi za Marekani dhidi ya Iran. Katika taarifa zake za karibuni, Trump amedai kuwa alikusudia kupunguza vikwazo dhidi ya Iran, lakini maneno ya Kiongozi Muadhamu yamezuia uamuzi huu. Madai haya ya kitoto si tu hayana kweli wowote, bali pia yanaonyesha hana uelewa wa kutosha kuhusu hali ya Iran na watu wake.

Jumuiya ya kimataifa inajua wazi kwamba siasa za Trump kuhusu Iran haziongozwi kutokana na nguvu, bali na kukata tamaa. Tishio la wazi la Trump dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi sio tu ni ukiukaji wa wazi wa sheria na kanuni za kimataifa, bali ni mwanzo wa mchezo hatari. Trump anajua kuliko mtu mwingine yeyote kwamba kosa lolote la kistratijia kuhusu taifa la Iran linaweza kuifanya dunia nzima kutokuwa salama na kuwa kichinjio cha wavamizi na washirika wao. Hili sio tishio, bali ni ukweli ambao watawala wa Marekani na Israel wanauelewa vizuri.

Kinachosikika leo katika maneno ya kichochezi ya Trump si msimamo wa mwanasiasa mwenye nguvu, bali ni jaribio la mchezaji aliyeshindwa kuficha hasira na kushindwa kwake. Mchezo na Iran, hapana!

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha