Takwimu hizo zimetolewa katika utafiti mpya ulioongozwa na Profesa Michael Spagat, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha London, pamoja na Profesa Khalil Shikaki, mtaalamu wa siasa kutoka Palestina. Utafiti huo ulihusisha uchunguzi wa kaya 2,000 katika Ukanda wa Gaza ulioko chini ya mzingiro, zenye jumla ya watu karibu 10,000.
Kwa mujibu wa utafiti huo, hadi kufikia Januari 2025, watu wapatao 75,200 walipoteza maisha kwa njia ya kikatili wakati wa uvamizi wa Israel, wengi wao wakiwa wameuawa na silaha za kivita za Israel. Aidha, vifo 8,540 vilitokana na njaa, maradhi, na mazingira duni ya kibinadamu, na hayo yote yamesababishwa na hujuma ya utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo hilo.
Tangu Januari, Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti zaidi ya vifo 10,000, na hivyo kupelekea idadi ya jumla ya waliouawa kufikia karibu 100,000.
Takwimu hizi mpya zinaonesha kwamba idadi halisi ya vifo ni kubwa zaidi ya ile iliyokuwa inaripotiwa rasmi, huku hali hiyo ikizidi kudhoofishwa na baa la njaa, maambukizi ya magonjwa, na mashambulizi ya risasi katika vituo vya usambazaji chakula.
Profesa Spagat alisema kuwa data ya utafiti huo “inaweka vita vya Gaza miongoni mwa migogoro yenye umwagaji damu mkubwa zaidi katika karne ya 21.”
Aidha aliongeza kuwa kiwango cha waliouawa ikilinganishwa na idadi ya watu wa Gaza ni cha juu mno , takriban asilimia 4 ya wakazi.
Ameongeza kuwa: “Sijui kama kuna tukio lingine katika karne hii ya 21 ambalo limefikia kiwango hicho.”
Kwa mujibu wa watafiti hao, asilimia 56 ya waliouawa ni wanawake na watoto walio na umri wa miaka 18 au chini. Idadi hii ni zaidi ya mara mbili ya kiwango kilichoshuhudiwa katika mizozo mingi ya kisasa duniani.
Israel ilianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya kundi la kupigania ukombozi la Palestina,Hamas, kutekeleza operesheni ya kihistoria dhidi ya utawala wa Kizayuni, ikiwa ni kujibu ukatili uliokithiri wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Licha ya kusababisha maangamizi makubwa kwa maisha ya Wapalestina, utawala wa Tel Aviv haujafaulu kufikia malengo yake ya kuangamiza Hamas na kuwaachilia mateka walioko Gaza.
“Israel imeshindwa katika malengo yake ya kivita, lakini imeacha majeraha ya kudumu katika historia ya kibinadamu ya Gaza,” walisema wataalamu hao.
Your Comment