Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Riziki na kipato kwa hakika kiko mikononi mwa nani? Kwa mtazamo wa tauhidi, kila kitu kiko mikononi mwa Mwenyezi Mungu; lakini katika maisha ya kila siku, inaonekana kana kwamba wanadamu ndio wanaoamua riziki za wao kwa wao: mfanyakazi humtegemea mwajiri, mtumishi wa umma hulitegemea dola, na mtoto huwategemea wazazi. Basi ukweli wa jambo hili ni upi? Mtazamo sahihi na wa kina ni upi?
Neno “riziki” kiasili humaanisha kipawa na fungu linalomfikia mwanadamu (1), na halijifungi tu kwenye chakula na mavazi; bali kila kitu ambacho mwanadamu hunufaika nacho—kama elimu, heshima, hadhi, na uongofu—pia huhesabiwa kuwa ni aina ya riziki (2). Kwa mtazamo wa dini, Mwenyezi Mungu si Muumba wa ulimwengu pekee, bali pia ndiye Mruzuku wa kweli wa viumbe vyote. Qur’ani Tukufu imesisitiza ukweli huu mara nyingi: “Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mruzuku, Mwenye nguvu na uwezo madhubuti” (3), na “Je, yupo muumba mwingine asiye Mwenyezi Mungu anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini?” (4). Pamoja na hayo, katika aya nyingine, wanadamu pia wameelezwa kuwa wako katika nafasi ya kutoa riziki; kama baba anayewajibika kugharamia chakula na mahitaji ya mama katika kipindi cha kunyonyesha (5). Uhusishaji huu wa aina mbili wa riziki—kwa mtazamo wa nje unaonekana tofauti—lakini kwa hakika unaendana na kuafikiana (6).
Nukta ya Kwanza: Mtazamo wa Tauhidi
Katika mtazamo wa tauhidi, Mwenyezi Mungu si Muumba wa ulimwengu pekee, bali pia ni Msimamizi na Mwendeshaji wa mambo yote. Baadhi ya watu katika historia walidhani kwamba Mwenyezi Mungu aliuumba ulimwengu kisha akaacha uendeshaji wake mikononi mwa nguvu kama malaika, miili ya angani au viumbe wengine. Hata hivyo, Qur’ani Tukufu inalikanusha wazo hili kwa uwazi na kusema: “Yeye ndiye anayesimamia mambo (ya ulimwengu)” (7). Hivyo basi, mikondo yote ya uhai—kuanzia mienendo ya nyota hadi kuwafikishia waja riziki—iko chini ya uangalizi wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Uruzuku ni sehemu ya ule ulezi (rububiyya) na usimamizi wa Mwenyezi Mungu. Mtu yeyote akidhani kuwa kuna mwingine anayetoa riziki kwa uhuru na kwa kujitegemea, kwa hakika amemshirikisha Mwenyezi Mungu katika cheo cha Ulezi. Kwa hivyo, kuamini tauhidi ya rububiyya kunamaanisha kuamini kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mruzuku wa kweli na Msimamizi kamili wa uhai.
Nukta ya Pili: Mfumo wa Msururu wa Sababu (Nidhamu ya Urefu wa Visababishi)
Katika mtazamo wa tauhidi, hakuna kiumbe chochote ulimwenguni kinachofanya jambo kwa kujitegemea. Kama vile uwepo wa kila kiumbe unavyomtegemea Mwenyezi Mungu, ndivyo pia athari na vitendo vyake hutimia kwa idhini na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Kanuni hii huitwa tauhidi ya vitendo (tawḥīd al-af‘āl). Sababu na visababishi vyote ni pete za mnyororo wa wima ambao mwisho wake huungana na Mwenyezi Mungu, Kisababishi cha visababishi vyote. Baba, mwajiri au dola, japokuwa kwa dhahiri huonekana kuwa ni watoa riziki, kwa hakika ni visheni tu katika njia ya riziki ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, utoaji wa riziki unaofanywa na wanadamu hauko sambamba (sawa) na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, bali uko chini na ndani ya mapenzi Yake. Kama vile mwezi unavyorudisha mwanga wa jua, ndivyo mwanadamu anavyosambaza mng’aro wa fadhila ya Uruzuku wa Mwenyezi Mungu. Kwa maana hii, Mwenyezi Mungu ndiye Mruzuku kwa asili (bil-dhāt) na wengine ni waruzuku kwa kutegemea (bil-ghayr); yaani, chochote kinachofika kupitia mikono ya waja ni taswira ya riziki ya Mwenyezi Mungu inayopita kupitia wao kwenda kwa wengine (8).
Mwisho
Kwa mtazamo huu, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mruzuku wa kweli, lakini desturi Yake ni kwamba riziki ya mwanadamu ipatikane kupitia sababu za kimaumbile na juhudi za mtu binafsi na za kijamii. Kuelewa kwa usahihi ukweli huu huzaa matunda mawili yenye thamani kubwa:
Kwanza, huleta utulivu na amani moyoni mwa mwanadamu; kwa sababu anatambua kwamba riziki yake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, na hakuna yeyote anayeweza kwa uhuru kuipunguza au kuiongeza. Imani hii huimarisha tawakkul (kumtegemea Mwenyezi Mungu) na kuondoa utegemezi kwa wasiokuwa Yeye.
Pili, mtazamo huu haumzuii mwanadamu kufanya juhudi; bali humhamasisha kufanya kazi, kuwajibika na kuwasaidia wengine. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu amependa riziki ipite kupitia juhudi hizo. Hivyo, yule anayefanya kazi kwa ajili ya familia au jamii yake, kwa hakika ni chombo cha kufikisha rehema ya Mwenyezi Mungu. Mtazamo wa tauhidi unakusanya pamoja tawakkul na juhudi; ni mtazamo unaozitambua sababu za kimaumbile, huku pia ukitambua Chanzo cha msingi cha yote hayo kuwa ni Mwenyezi Mungu (9).
Tanbihi (Marejeo)
- Raghib al-Isfahani, Hussein bin Muhammad, Mufradāt Alfāẓ al-Qur’ān, Beirut, Dar al-Qalam, 1412 H, uk. 351.
- Jawadi Amoli, Abdullah, Tasnīm, tahqiq Ali Islami na Abdulkarim Abedini, Qum, Asra, 1389 SH, juz. 13, uk. 600; Ibn Manzur, Muhammad bin Makram, Lisān al-‘Arab, Beirut, Dar Sader, 1414 H, juz. 10, uk. 115.
- Surat adh-Dhāriyāt, Aya 58: “Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mruzuku, Mwenye nguvu na uwezo madhubuti.”
- Surat Fāṭir, Aya 3.
- Surat an-Nisā’, Aya 5.
- Jawadi Amoli, Abdullah, Tafsiri ya Kimaudhui ya Qur’ani Tukufu – Tauhidi katika Qur’ani, Qum, Asra, 1383 SH, uk. 430–432.
- Surat ar-Ra‘d, Aya 2.
- Subhani, Ja‘far, Misingi ya Tauhidi kwa mtazamo wa Qur’ani, Qum, Tawhid, 1361 SH, uk. 146–247.
- Kwa kusoma zaidi: Salawati, Azam na wengine, Uchambuzi wa Misingi ya Tauhidi katika Uruzuku, Jarida la Utafiti wa Kidini, Masika na Kiangazi 1401 SH, Toleo la 44, uk. 239–254.
Your Comment