19 Desemba 2025 - 16:53
Upinzani wa Iraq: Hatutokabidhi silaha zetu, na tunasimama imara dhidi ya shinikizo la Marekani

Haider Al-Khayoun, mhadhiri wa siasa za kimataifa, alibainisha kuwa vitisho vya Marekani na Israel dhidi ya Iraq si vipya, lakini kwa sasa vimekuwa tata zaidi kutokana na ukosefu wa serikali thabiti yenye uwezo wa kuchukua maamuzi ya kimkakati. Alisisitiza kuwa Iraq ni sehemu ya mlinganyo mpana wa kikanda unaojumuisha Iran, Syria, Lebanon na Gaza, na kwamba kuongezeka kwa mvutano katika maeneo hayo kuna athari za moja kwa moja kwa Baghdad.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein, ametoa onyo kali kuhusu kuendelea kwa vitisho vinavyotolewa na Marekani na Israel dhidi ya nchi yake, akisisitiza kuwa Iraq ni miongoni mwa mataifa yaliyoathiriwa zaidi na mvutano unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

Akizungumza katika mazingira ambayo shinikizo la kimataifa - hasa kutoka Marekani - limeongezeka kwa lengo la kuundwa kwa serikali “yenye msimamo wa kati” mjini Baghdad, Fuad Hussein alisema kuwa mvutano wa kisiasa bado haujafikia makubaliano ya mwisho kuhusu mihimili mitatu ya uongozi wa nchi. Alifafanua kuwa makundi ya upinzani wa silaha yana uwakilishi ndani ya Bunge la Iraq na yanacheza nafasi muhimu ya kisiasa na kiusalama, akisisitiza kuwa suala lao ni la ndani ya Iraq.

Ingawa Waziri huyo alikanusha kuwepo kwa masharti ya moja kwa moja kutoka Marekani, wachambuzi wa kisiasa wanaamini kuwa bado kuna shinikizo zisizo za wazi pamoja na ujumbe mbalimbali unaoifikia serikali ya Baghdad.

Kwa upande mwingine, mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani wa Iraq alinukuliwa na gazeti la Al-Akhbar akisema:
“Hatutokabidhi silaha zetu kamwe, wala hatutasalimu amri kwa matakwa ya Marekani au shinikizo lolote la kisiasa au kiuchumi.”
Aliongeza kuwa makundi ya upinzani yana uungwaji mkono wa wananchi na uwakilishi madhubuti bungeni, na yako tayari kukabiliana na tishio lolote kutoka Marekani au Israel.

Aidha, Ali Muhyiddin, Mkurugenzi wa Kituo cha Al-Ghad cha Tafiti za Kimkakati, alisema kuwa onyo la Waziri wa Mambo ya Nje linategemea taarifa sahihi za kidiplomasia. Alieleza kuwa vitisho hivyo vimetolewa na baadhi ya maafisa wa Marekani kama Mark Savaya na Tom Barrack, na vinaweza kuwa vya kijeshi, kiusalama, kiuchumi au kisiasa. Kwa mujibu wake, shinikizo hizo ni sehemu ya mpango mpana wa kudhoofisha nafasi ya Iraq na makundi ya upinzani katika mizani ya kuzuia nguvu (deterrence) ya kikanda.

Naye Haider Al-Khayoun, mhadhiri wa siasa za kimataifa, alibainisha kuwa vitisho vya Marekani na Israel dhidi ya Iraq si vipya, lakini kwa sasa vimekuwa tata zaidi kutokana na ukosefu wa serikali thabiti yenye uwezo wa kuchukua maamuzi ya kimkakati. Alisisitiza kuwa Iraq ni sehemu ya mlinganyo mpana wa kikanda unaojumuisha Iran, Syria, Lebanon na Gaza, na kwamba kuongezeka kwa mvutano katika maeneo hayo kuna athari za moja kwa moja kwa Baghdad.

Wakati huo huo, ripoti zinaonyesha kuwepo kwa shinikizo za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutoka Marekani, ikiwemo vitisho vya vikwazo vya kiuchumi na kisiasa endapo makundi ya upinzani yatashiriki katika serikali ijayo. Vyanzo vya kisiasa vimeripoti kuwa ujumbe wazi umetumwa kwa viongozi wa Mfumo wa Uratibu (Coordination Framework) ukihimiza uteuzi wa Waziri Mkuu “wa wastani”.

Shinikizo hizi zinaambatana na hofu ya kuwekewa vikwazo vya kifedha, hususan katika masuala ya dola ya Marekani, sekta ya nishati, na ushirikiano wa kiusalama. Aidha, Bunge la Marekani (Congress) katika Sheria ya Uidhinishaji wa Ulinzi kwa mwaka wa fedha 2026, limeweka masharti ya kupunguza sehemu ya msaada wa kiusalama kwa Baghdad iwapo uwezo wa kiutendaji wa makundi yasiyounganishwa rasmi katika taasisi za serikali hautapunguzwa.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha