Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- katika kongamano la “Maktaba ya Soleimani; busara ya muqawama na mustakabali wa kambi ya haki”, Sayyid Abdulqadir Alusi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Ribat Muhammadi Iraq, akirejea hali hatarishi ya ulimwengu wa Kiislamu, alisisitiza kuwa Shahidi Luteni Jenerali Haj Qasem Soleimani na Shahidi Abu Mahdi Al-Muhandis, katika wakati wa hatima wa historia ya Umma wa Kiislamu, kwa kujitolea na jihadi yao, waliunda kizuizi kisichopenyeka dhidi ya miradi ya Kizayuni, Kimarekani na kitakfiri, na kuzuia kuangamizwa kwa utambulisho wa kidini, ustaarabu na utu wa Umma wa Muhammad (s.a.w.w).
Alusi, akianza kwa kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumtakia rehema Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt wake watukufu, alisema: Umma wa Kiislamu leo uko katika moja ya hatua hatari na nyeti zaidi za kihistoria; hatua inayoshuhudia uvamizi wa Kizayuni wa ardhi na vitakatifu vya Kiislamu, uvamizi wa kijeshi wa Marekani, pamoja na fitna za kikabila na kimadhehebu zinazotishia uhai wa Umma.
Aliongeza: Katika mazingira haya yaliyojaa uadui na chuki dhidi ya Uislamu, Mwenyezi Mungu huwainua wanaume wakubwa kwa ajili ya kuutetea Umma; wanaume wa imani, kujitolea na kujifia, wanaolinda uhai, utambulisho na malengo makubwa ya Umma wa Kiislamu kwa damu na nafsi zao.
Njia hii ndiyo njia ya Manabii, Mitume, Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s) na mawalii wa Mwenyezi Mungu, ambao kila dini, maadili na uwepo wa Umma ulipokuwa hatarini, waliingia uwanjani.
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Ribat Muhammadi Iraq, akibainisha nafasi ya mashahidi wa muqawama, alisema: Katika zama zetu, bendera hii ilibebwa na Shahidi mkubwa Haj Qasem Soleimani na Shahidi shujaa Abu Mahdi Al-Muhandis.
Walisimama katika wakati muafaka na kwenye nukta nyeti ya historia ili kuzuia miradi iliyolenga kuuangamiza Umma wa Muhammad. Maadui, kwa kuunda na kuunga mkono makundi ya kitakfiri kama Al-Qaeda na Daesh (ISIS), walikusudia kuingiza nchi za Kiislamu katika machafuko na kuvunja upinzani wowote wa wananchi ili kudhibiti mustakabali wa Umma.
Aliendelea: Makundi haya ya kitakfiri yalikuwa zana mikononi mwa wavamizi, hususan Marekani; lakini uwepo wa moja kwa moja uwanjani na uongozi wenye busara wa Shahidi Soleimani na Shahidi Al-Muhandis uliharibu mipango hiyo.
Kwa jihadi na kujitolea kwao, kuanzia Palestina na Gaza yenye kusimama kidete hadi Syria na Iraq zilizojeruhiwa na kuvamiwa, walisimama mstari wa mbele na hawakuruhusu mradi wa kuangamiza utambulisho wa Kiislamu na kibinadamu wa mataifa haya kufanikiwa.
Alusi akisisitiza athari za kimkakati za muqawama, alisema: Uwepo na uongozi huu wa kipekee uliigeuza Iraq, Gaza na miji mingine ya muqawama kuwa ngome za kushindwa kwa miradi ya kibabe, na kuifanya Umma wa Kiislamu leo kujitokeza katika mapambano haya ukiwa na nguvu na uimara zaidi kuliko hapo awali.
Mradi wa Muqawama wa Kiislamu sasa umekuwa uhalisia wa uwanjani wenye athari, ambao adui analazimika kuuhesabu.
Akiyafananisha mapambano haya na “futuwwa ya Kiungu”, alisema: Jihadi hizi ni mwendelezo wa njia ya Nabii Ibrahim (a.s); futuwwa ile ile iliyosimama dhidi ya masanamu, na leo inasimama dhidi ya masanamu ya kisasa ya taghuti, ubeberu wa kimataifa na watawala wanaodhibiti hatima za watu.
Shahidi Soleimani na wenzake, kwa kuyavunja masanamu haya, waliandaa njia ya heshima na izza kwa Umma.
Mwisho, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Ribat Muhammadi Iraq alisisitiza: Futuwwa - (Ushujaa wa Roho na Tabia njema) - hii ni ya Kiungu na ya Mola, ambayo Mwenyezi Mungu ameikadiria kwa Waumini. Mashahidi wa muqawama ni mashahidi wa ushindi wa Umma; wanaume ambao kwa damu yao waliandika upya historia ya Umma wa Kiislamu katika zama hizi, na kuchora njia ya heshima, utu na ushindi kwa vizazi vijavyo.
Your Comment