Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, amefanya ziara Zanzibar akielekea Kizimkazi kwa ajili ya kutoa mkono wa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia msiba wa kuondokewa na mumewe, Marehemu Hafidh Ameir Hassan.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya kuonyesha mshikamano na kutoa pole kwa Rais Samia pamoja na familia yake katika kipindi hiki cha majonzi. Marehemu Hafidh Ameir Hassan alikuwa mume wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika safari hiyo, msafara wa viongozi wa TIC ulipata fursa ya kupitia katika Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyopo Kisiwandui, Zanzibar, ambapo viongozi hao walisaini katika Daftari la Wageni kabla ya kuendelea na safari kuelekea Kizimkazi.
Msafara huo uliongozwa na Sheikh Mkuu wa TIC, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, akiambatana na Makamu wake, Samahat Sheikh Mohamed Abdi; Makamu Mwenyekiti, Abdulkarim Shamte; Katibu, Nyello; pamoja na Naibu Katibu wa Wanawake wa TIC, Kijoli Jumaa Wema.
Viongozi hao waliambatana pia na mwenyeji wao, Hesmen Haloo, katika safari hiyo ya kuelekea Kizimkazi.
Ziara hiyo inaendelea kuonyesha nafasi ya Jumuiya ya Shia Tanzania katika kushirikiana na viongozi na jamii kwa nyakati mbalimbali, hususan wakati wa misiba na changamoto zinazowakabili wananchi.
Rais Samia Suluhu Hassan alizaliwa Kizimkazi, Zanzibar, eneo ambalo pia limekuwa sehemu muhimu katika historia yake binafsi.
TIC inaendelea kutoa pole na kuungana na Rais Samia pamoja na familia yake katika kipindi hiki cha majonzi, huku ikiwaombea subira na moyo wa ustahimilivu katika kukabiliana na msiba huo.
Maoni yako