Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo katika hafla ya kupokea hati za utambulisho kwa nyakati tofauti za mabalozi wapya wa Sudan, Denmark, Niger, Ujerumani, Qatar na Norway hapa mjini Tehran na kukosoa vikali kimya cha madola ya Magharibi kwa mauaji yanayofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia yoyote.
Rais Pezeshkian amegusia kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon na kusema kuwa, kwa bahati mbaya, tunashuhudia utekelezwaji wa misimamo ya kindumakuwili ya Marekani na nchi za Ulaya kuhusiana na suala la haki za binadamu.Amesema, wakati nchi hizo zikiusumbua ulimwengu mzima kuhusiana nasuala la ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi kama Iran, leo zimenyamazia kimya mauaji ya makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia yanayofanywa na utawala wa Kizayuni hatua ambayo ni kupiga muhuri wa kuidhinisha na kuunga mkono jinai hizo.
Katika mazungumzo yake na balozi mpya wa Qatar hapa mjini Tehran ameshukuru juhudi za nchi hiyo ya Kiarabu kwa ajili ya kusimamisha vita na kusema: Lau nchi za Kiislamu zingekuwa na umoja na kuulalamikia kwa pamoja na kuchukua hatua kwa sauti moja dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni, tusingekuwa tunashuhudia mwendelezo wa kifidhuuli kama huu wa vitendo vya jinai vya utawala huu.
342/