10 Agosti 2020 - 09:21
Guterres katika kumbukumbu ya Nagasaki: Silaha zote za nyuklia ziangamizwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia maadhimisho ya miaka 75 tangu bomu la atomiki lilipodondoshwa katika mji wa Nagasaki, Japan, amesema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kufanikisha ulimwengu usiokuwa na silaha za nyuklia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katibu Mkuu Guterres ametahadharisha kuwa pamoja na uvumilivu wa watu wa Nagasaki matarajio ya matumizi ya silaha za nyuklia kwa makusudi au kwa bahati mbaya ni ya hatari ya juu.

Amefafanua kuwa kwa kadri silaha za nyuklia zinavyoboreshwa kuwa za kisasa, ngumu, za haraka na hatari zaidi, uhusiano kati ya nchi zenye silaha za nyuklia unaelezewa kuwa wa kutokuaminiana, ukosefu wa uwazi na pia ukosefu wa mazungumzo. 

Guterres amesema mafanikio katika usitishaji wa silaha za nyuklia yako hatarini na kuongeza kuwa, “hali hii ya kutisha inapaswa kubadilishwa.” 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasifu waathirika wa shambulio la bomu la nyuklia huko Nagasaki, ambao wamegeuza shida yao ya miongo kadhaa kuwa onyo juu ya hatari ya silaha za nyuklia.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 6 Agosti 1945, ndege ya kivita ya jeshi la Marekani aina ya B-29 ilidondosha bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima nchini Japan kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani, Harry Truman. Baada ya siku tatu, yaani 9 Agosti 1945, Marekani ilidondosha bomu jingine la atomiki katika mji wa Nagasaki. Ingawa mabomu hayo angamizi yalipelekea Japan isalimu amri katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia lakini yalipelekea kupoteza maisha raia zaidi ya 220,000.

Marekani ambayo ni nchi pekee kuwahi kutumia silaha za atomiki dhidi ya raia ingali inaendelea kudai kuwa inatetea haki za binaadamu na wakati huo huo pia inazidi kuimarisha uzalishaji mabomu hatari ya atomiki.

342/