Kwa mujibu wa televisheni ya Al Manar, Sheikh Naim Qassem ameyasema hayo katika taarifa ramsi na kuongeza kuwa Hizbullah inasimama pamoja na Iran katika kukabiliana na uharamu wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni donda la saratani na madhalimu wengine duniani.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, “Tunasisitiza nafasi yetu ya kuwa pamoja na Iran, uongozi wake na watu wake na tutachukua hatua zinazofaa katika kukabiliana na hujuma ya kinyama ya Marekani na utawala wa Kizayuni.
Taarifa hiyo imekuja baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutekeleza hujuma ya kichokozi dhidi ya Iran Ijumaa iliyopita ambapo ulilenga maeneo ya kijeshi na kiraia ya Iran. Katika kujibu, Iran inaendelea kulipiza kisasi kwa kutekeleza Operesheni Ahadi ya Kweli III kwa kulenga ngome za kijesi na kijasusi za Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Sheikh Qassem amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwanga wa matumaini duniani kwani inawasaidia watu wanaodhulumiwa. Ameongeza kuwa madhalimu dunani, hasa Marekani, hawawezi kustahamili mfumo wa kibinadamu wa Iran na kwamba hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kama kiongozi wa mataifa huru na yanayojitegemea duniani.
Amesisitiza: “Utawala wa kiimla wa Markeani na utawala utendao jinai wa Israel hawawezi kulazimu taifa la Iran lisalimu amri.”
Aidha amesema kuwa: “Mpango wa nyuklia wa Iran una malengo ya amani na unalenga kudhamini maslahi ya taifa la Iran kwa mujibu wa sheria za kimataifa.”
Kiongozi wa Hizbullah ameashiria matukio ya hivi karibuni ambayo yameonyesha udhaifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na hasara kubwa ambazo utawala huo umepata katika miaka yake 77 ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kuongeza kuwa , Israel imelazimika kuomba msaada wa haraka wa Marekani katika kukabiliana na opereseni za kijeshi za Iran.
342/
Your Comment